1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Umoja wa mataifa kuhusu malengo ya maendeleo ni miongoni mwa mada zilizomulikwa magazetini

Oumilkher Hamidou20 Septemba 2010

Wahariri wamechambua pia maandamano ya umma dhidi ya kurefushwa muda wa kutumiwa nishati ya kinuklea humu nchini na mkutano wa Umoja wa mataifa kuhusu malengo ya Milenia

https://p.dw.com/p/PH88
Makao makuu ya Umoja wa mataifa mjini New-YorkPicha: AP

Tuanzie lakini New York unakoanza hii leo mkutano wa viongozi wa Umoja wa mataifa kuhusu malengo ya maendeleo ya millenia.Gazeti la "General Anzeiger" la mjini Bonn linaandika:

Miaka mitano kabla ya muda uliowekwa kumalizika kimoja ni dhahir:machache tuu kati ya malengo manane ya Millenia yaliyowekwa na Umoja wa mataifa ndio yatakayoweza kufikiwa.Ni jambo la kusikitisha.Suala hili linahusu mustaqbal wetu wenyewe:Ulimwengu ambao mamilioni ya watu wanalazimika kuishi katika hali ya umaskini na bila ya elimu,ambako mazingira yanaendelea kuchafuliwa na wakaazi wake wanaongezeka bila ya mpangilio si ulimwengu salama.Na ni kashfa pia kuona kwamba kila sekondi sita mtoto mmoja mdogo anakufa kutokana na ukosefu wa chakula bora na njaa.

Hayo ni maoni ya gazeti la General Anzeiger kuhusu mkutano wa Umoja wa mataifa kutathmini malengo ya maendeleo ya millenia mjini New-York,miaka mitano kabla ya muda uliowekwa kukamilika.Mada yetu ya pili magazetini hii leo inahusiana na uchaguzi nchini Afghanistan.Na gazeti la "Nordsee-Zeitung" la mjini Bremerhaven linaandika:

Matumaini nchi za magharibi waliyo yapigia upatu baada ya kuuwawa watu 46 tu wakati wa uchaguzi,yalilengwa kitu kimoja tuu:kujipendekeza kwa wapiga kura nyumbani.Hakuna badala ya kufunga virago-ndio kauli mbiu.Kwamba juhudi zote za kuleta uhuru,kushirikishwa wakinamama na kuleta amani zimeshindwa nchini Afghanistan-hakuna anaependelea kusema kwa sauti ya juu.Kila watu wanaposifu uchaguzi huo ambao kwa mara ya kwanza umesimamiwa na wenyewe waafghanistan,ndipo walimwengu nao watakapojitakasa nyoyo zao,wakati utakapowadia.Vurugu likitokea,watakaobeba jukumu sio wengine bali wenyewe waafghanistan.

Protest gegen Atomkraft in Berlin Dossierbild 2
Malalamiko ya umma mjini Berlin dhidi ya nishati ya kinukleaPicha: picture alliance/dpa

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na hasira za wajerumani dhidi ya kurefushwa muda wa kutumiwa vinu vya nishati ya kinuklea.Gazeti la "Der neue Tag" la mjini Weiden linaandika:

Yadhihrika kana kwamba tunarejea katika zile enzi za maandamano dhidi ya vinu vya kinuklea vya Wackersdorf au Gorleben .Serikali ilificha baadhi ya mambo ilipotangaza kurefusha muda wa vinu vya nishati ya kinuklea.Kwamba makubaliano yamefikiwa kichini chini,hali hiyo imewafanya wananchi waamini kwamba serikali haizingatii kikamilifu hofu zao.Mbinu kama hiyo,serikali ya muungano wa nyeusi na manjano,haipaswi kuirudia,mfano katika suala la kupatikana mahala pa kuhifadhiwa takataka za kinuklea.Kwasababu hali kama hiyo ikitokea tena,basi matokeo yatapelekea kuzidi makali lawama za umma na kusababisha matumizi ya nguvu.Na hali kama hiyo hakuna anaeitaka wakati huu tulio nao.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mpitiaji:Abdul-Rahman