Mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi Paris warefushwa
11 Desemba 2015Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius amekieleza kituo cha televisheni nchini Ufaransa kuwa atawasilisha waraka wa muafaka mpya wa makubaliano ya kupambana na kupanda kwa ujoto siku ya Jumamosi asubuhi, akilenga kupatikana kwa makubaliano miongoni mwa karibu mataifa 200 ifikapo mchana kesho, na sio leo kama ilivyopangwa hapo kabla.
"Tunasonga mbele lakini kuna kazi kubwa mbele yetu. Kwa hiyo leo waraka utafanyiwa kazi, nitaendelea na mashauriano. Kwa hiyo nitawasilisha waraka sio Ijumaa jioni , kama nilivyofikiri, bali mapema Jumamosi asubuhi na tutaweza kuchukua maamuzi muhimu mchana."
Lakini ameongeza kuwa hali ya mahusiano ni nzuri, mambo yanakwenda vizuri, na yanakwenda katika mwelekeo sahihi. Mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi mara kadhaa huendelea hadi katika mwisho wa juma.
Hali ni nzuri lakini ngumu
Mazungumzo hayo yaliyoanza Novemba 29, yalitarajiwa kumalizika leo Ijumaa(11.12.2015).
Usiku wa kuamkia Ijumaa ulikuwa mgumu sana, chanzo kimoja kimesema. Mazungumzo yaliyofanyika usiku yameonesha kuendelea kwa mivutano kuhusu masuala kama vipi kuweka uwiano katika hatua za mataifa tajiri na masikini kupunguza gesi zinazoharibu mazingira na pia malengo ya muda mrefu ya makubaliano ya aina yoyote ya kuweka ukomo wa utoaji wa gesi hizo, duru hiyo imesema.
Kwa upande wake, rais wa China Xi Jinping na rais wa Marekani Barack Obama walizungumza kwa simu na kusema nchi zao zitaendeleza ushirikiano katika mabadiliko ya tabia nchi, imeripoti televisheni ya taifa ya China.
Jioni ya jana Alhamis(10.12.2015) waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius aliwasilisha mswada wenye kurasa 27 ambao umepunguzwa kiasi na kuondolewa baadhi ya vipengee muhimu vinavyoleta mivutano.
Wataalamu walalamika
Wakati huo huo wataalamu wa masuala ya haki za binadamu wamewataka mawaziri katika mkutano huo kulirejesha suala la kuheshimu haki za binadamu katika sehemu ya suala la lazima katika mswada mpya wa makubaliano ya dunia ili kupambana na ongezeko la ujoto duniani, baada ya kuondolewa kutoka katika waraka wa kwanza jioni jana Alhamis.
Mashirika ya haki za binadamu, mashirika ya kutoa misaada na watu walioathirika na mabadiliko ya tabia nchi wamekatishwa tamaa kuona pendekezo la awali la kushurutisha utekelezaji , ambalo lilisema makubaliano ya Paris ni lazima kutekelezwa "kwa misingi ya heshima ya haki za binadamu" limeondolewa.
Asubuhi jana , wataalamu wa Umoja wa mataifa wamesema haki za binadamu tayari zinakiukwa kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, ikiwa ni pamoja na hali mbaya ya hewa , inayosababisha majanga na kupanda kwa viwango vya maji ya bahari, pamoja na suluhisho.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Daniel Gakuba