1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kimataifa wa mazingira waanza Nairobi

28 Februari 2022

Mamia ya wajumbe kutoka nchi mbalimbali kote ulimwenguni wamekutana  jijini Nairobi kuhudhuria kikao cha tano cha mkutano wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA)

https://p.dw.com/p/47jOm
Schweiz UN l Bericht zur Erreichung der Klimaziele - Inger Andersen, John Christensen , Petteri Taalas
Picha: picture alliance/dpa/Keystone/S. di Nolfi

Mkutano huo ambao unafanyika katika mazingira ya kipekee kutokana na janga la COVID-19 umeandaliwa rasmi katika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira (UNEP). Inger Andersen ni mkurugenzi mkuu wa Shirika la UNEP. "Swala kuu katika linalojitokeza katika mkutano huo wa Baraza la UNEA ni kuhusu taka za plastiki. Tunayo mataifa 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa ambao wamepitisha maazimio yanayolenga kubuni makubaliano mwafaka ya kutokomeza taka za plastiki kwa kupunguza matumizi yake kutoka vyanzo vyake hadi baharini.”

Wajumbe hao, wakiwepo mawaziri, wanadiplomasia na wanaharakati kutoka makundi ya kutetea uhifadhi wamazingira wanapania kufikia maamuzi ya pamoja katika hatua za mwanzo za kukabiliana na tatizo sugu la uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka za plastiki.

Senegal Symbolbild Plastikmüll im Meer
Taka za plastiki ni donda sugu ulimwenguniPicha: picture alliance/dpa/N. Bothma

Matumizi ya plastiki yanachangia pakubwa katika uchafuzi wa mazingira. Kulingana na Shirika la UNEP zaidi ya chupa za plastiki milioni moja hununuliwa kila dakika kote ulimwenguni kwa matumizi ya maji ya kunywa, ilhali mifuko ya plastiki zaidi ya trilioni 5 hutumiwa kila mwaka kote duniani.

Andersen, aliye raia wa Denmark, anasema ana matumaini kuwa mkutano wa baraza la UNEA unafikia suluhu la kudumu. "Tunataraji kuwa mkutano wa UNEA utafikia maamuzi ya kihistoria katika kukabiliana na swala la taka za plastiki kama vile makubaliano ya Paris yalivyokuwa kwa mabadiliko ya tabia nchi.”

Hans Brattskar, mjumbe maalum kutoka Wizara ya Mazingira ya Norway, amesema ana imani kwamba washiriki katika mkutano huo wataweza kufikia maafikiano mwafaka.

Wajumbe kutoka mataifa 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa wanashiriki katika mkutano huo jijini Nairobi.

Wakati wa ufunguzi rasmi, wasemaji wa mkutano huo wamekemea vikali hatua ya Russia kuivamia kijeshi nchi ya Ukraine na kuitaka jumuia ya kimataifa kuingilia kati ili kukomesha vita hivyo.

Reuben Kyama/DW-Nairobi