1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa kunusuru bahari wafanyika Ufaransa

11 Februari 2022

Viongozi wa dunia wamekutana katika pwani ya Atlantiki ya Ufaransa katika mji wa Brest ili kujadili hatua za kuilinda bahari dhidi ya vitisho kama uvuvi kupita kiasi na uchafuzi wa plastiki.

https://p.dw.com/p/46tT7
Plastikmüll im Meer
Picha: Agung Parameswara/Getty Images

Mkutano huo uliopewa jina la "One Ocean summit" unakuja wakati mamlaka za Ulaya zikifanya uchunguzi kuhusu dampo kubwa la samaki katika ghuba ya Gascogne ambayo wanaharakati wa mazingira wanasema ni unyanyasaji unaofanywa na meli kubwa ambazo huharibu mfumo wa ekolojia wa chini ya bahari.

Bahari inachukua nafasi ya zaidi ya asilimia 70 katika sayari hii, na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameandaa mkutano huo wa siku tatu katika mji wa Brest kwa msaada wa Umoja wa Mataifa. Macron amesema, kutachukuliwa maamuzi ambayo ana uhakika yatasaidia kuimarisha hatua zilizo muhimu.

Viongozi wengine wanahudhuria mkutano huo, ikiwa ni pamoja na Rais wa Misri Abdel-Fattah el-Sissi, ambaye nchi yake itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa mwaka huu, kiongozi wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen, Mjumbe Maalum wa Marekani kuhusu masuala ya hali ya hewa John Kerry na viongozi wengine kadhaa wa Afrika na Ulaya. Viongozi wengine watashiriki kwa njia za kimtandao.

Tansania Plastikflaschen am Strand
Raia akipita kando ya bahari ya Hindi TanzaniaPicha: Amas Eric in Dar es Salaam/DW

John Kerry amesema masaibu yanayotupata sote yanastahili kuzingatiwa. Ameongeza kuwa, kuna shughuli kubwa na za ajabu zinazoendelea kila kukicha baharini ambazo haziwezi kutofautishwa na uhalifu mkubwa unaofanywa na makampuni yaliyopo nchi kavu, ikiwa ni pamoja na vitendo vya utakatishaji fedha na ulaghai ili kuharibu juhudi nzuri za wavuvi duniani kote ambao wanajaribu kutii sheria. Shughuli haramu baharini zinakadiriwa kuchangia takriban humusi ya uvuvi duniani kote.

Kerry ameendelea kuwa Bahari ni muhimu kwa maisha yetu, hivo inahitaji kulindwa.

"Bahari ndiyo inayowezesha uhai duniani. Inazalisha zaidi ya nusu ya hewa safi tunayopumua, na ambayo pia iko hatarini. Zaidi ya asilimia 50 hadi 80 ya oksijeni hiyo hutoka baharini. Kwa hakika , bahari hutoa chakula na riziki kwa mabilioni ya watu.Na sisi sote tunaoijali bahari tumefika Brest kuweka ahadi kwamba huu lazima uwe mwaka ambao tunafanya kazi ya ziada kwa ajili ya wananchi wetu. Hii inaonyesha wazi uhusiano uliopo kati ya ulinzi wa hali ya hewa na ulinzi wa Bahari."

Katika taarifa ya pamoja, Ufaransa na Marekani zimesema zinaunga mkono kuanzishwa kwa mijadala kuhusu Mazingira katika Mkutano ujao wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa ili kushughulikia mzunguko kamili wa uwepo wa plastiki na kukuza uchumi shirikishi.