1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa hali ya hewa duniani huko Poland

Miraji Othman12 Desemba 2008

Hakuna maendeleo yaliopatikana huko Poznan katika mkutano wa kilele wa hali ya hewa duniani

https://p.dw.com/p/GF2x
Mkutano wa kilele wa hali ya hewa duniani huko Poznan, PolandPicha: DW / Böhme

Baada ya wiki mbili za mashauriano, mkutano wa 14 wa Umoja wa Mataifa juu ya hali ya hewa duniani umemalizika katika mji wa Poznan, Poland. Maamuzi barabara hayajafikiwa, mambo mengi yameachwa yabakie katika mwenendo wa mashauriano na kuahirishwa hadi mwakani. Kama kweli hapo Disemba mwakani kutafikiwa mjini Copenhagen, Denmark, mkataba wa dunia juu ya hali ya hewa, ni jambo linalonin'ginia bado.

Ni katika wakati wa nadra uliotokea katika mkutano huo wa hali ya hewa ya dunia mjini Poznan ambapo wawakilishi wa mkutano huo kutoka duniani kote wanaukumbuka: kwanini walikuweko katika mkutano huo? Walikumbushwa na tamko la waziri mkuu wa Tuvalu, kisiiwa kidogo sana kusini mwa Bahari ya Pasifik. Waziri mkuu huyo, Apisei Lelemia, alisema hivi: Sisi ni wananchi tunaojivuna, tunataka, kama wananchi na kama taifa kubaki tunaishi. Tuvalu, kama vile visiwa vingine na maeneo ya mwambao, kitatoweka, pindi jamii ya kimataifa haitakubaliana juu ya kupunguza sana hewa chafu angani.

Lakini nini kingine ambacho watu wa Tuvalu wafanye, pale sasa wanaposikia kwamba Mkutano wa Poznan haujaleta maendeleo katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani; wanaposikia kwamba nchi tajiri na wachafuzi wakubwa wa hewa hata hawajaweza kukubali kuandikwa katika hati juu ya tarakimu za malengo yanayowekewa katika kupunguza moshi hewani?

Pale mtu anaposoma vipi mabilioni ya Euro na dola za Kimarekani zilivotafunwa na wajanja katika taasisi za fedha duniani, na vipi fedha nyingi mno zimeingizwa ili kuudhibiti mzozo wa sasa wa kiuchumi duniani, basi mtu lazima awakubalie, tena bila ya kutia ati ati, wale watu wanaosema kwamba pindi matatizo ya hali ya hewa duniani hayatadhibitiwa, basi matokeo ya uharibifu wake yatakuwa makubwa zaidi kuliko mzozo huu wa sasa wa kifedha duniani.

Yule ambaye anashughulikia ulinzi wa hali ya hewa tu katika wakati uchumi unakwenda vizuri, na katika nyakati mbaya anasema kwamba hana fedha kwa ajili ya ulinzi wa hali ya hewa, basi mtu huyo hajayafahamu mabadiliko makubwa ya hali ya hewa yanayotokea duniani na ambayo yanaweza kusomwa katika ripoti za wataalamu.

Mwito uliotolewa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kwamba kuweko Maafikiano Mepya Duniani juu ya Ulinzi wa hali ya hewa inafaa usikilizwe. Sio kwamba mtu akichore kila kitu kwa rangi ya kijani, sio. Lakini katika fikra mtu inafaa awe huru kusema kwamba ulinzi wa mazingira ni msingi wa mipango ya kuukuza uchumi kote duniani. Na kwa wale mabepari waliobobea, huenda jambo hilo linawafaa, kwani linawaachia kupata faida. Kwa mfano, Ujerumani katika muda imeweza kufikia asilimia 15 ya mapato yake ya kiviwandani kutokana na ufundi wa ulinzi wa mazingira.

Katika mashauriano juu ya hali ya hewa duniani kuna mambo mawili muhimu, nayo ni imani na haki. Vipi nchi zinazoendelea zisiamini nchi za viwanda ambazo tangu miaka mitano ziliahidi kuweka malengo ya fedha katika kuleta uwiano juu ya suala la mabadiliko ya hali ya hewa duniani, na kila wakati kuna mazungumzo mepya juu ya jambo hilo na hakuna hata Euro moja iliotolewa? Na vipi juu ya nchi kama vile India,China, Brazil, Afrika Kusini zihisi juu ya msimamo wa kulegalega wa nchi za Ulaya? Wakati kuna nchi ambazo zimejitolea kupunguza uchafuzi wa hewa, ziko nyingine ambazo tayari ziko njiani kupotea sifa zao kama nchi zinazoongoza katika kupambana na uchafuzi wa mazingira duniani. Tutazamie kwamba Marekani baadae itachukuwa nafasi hiyo ya uongozi.

Kutokana na matokeo ya mkutano wa Poznan, kuna jambo moja wazi, nalo ni kwamba hakuna barabara kuu ilio wazi kuelekea Copenhagen, lakini kuna mashimo katika barabara hiyo, na kuna vituo vingi katikati. Ikiwa katika miezi ijayo hakutawezekana kuwa na safari ilio wazi na kuliweka suala la ulinzi wa mazingira juu katika ajenda, basi mkutano wa Copenhagen utawavunja moyo watu sana.