1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi juu ya nishati

Ramadhan Ali24 Mei 2006

Rais Vladmir Putin wa Urusi,anakutana leo na viongozi wa Umoja wa Ulaya huko Sotschi,Urusi katika kikao kilichogubikwa na mvutano juu uhakika wa kujipatia gesi kutoka kampuni la nishati la Urusi-GAZPROM.

https://p.dw.com/p/CHLU
Vladimir Putin
Vladimir PutinPicha: AP

Mkuu wa Tume ya Ulaya mjini Brussels, amekaribisha hatahivyo, dhamana iliotolewa na Urusi kwamba unaweza bila ya wasi wasi kutegemea gesi kutoka Urusi.

Mada ya kupewa uhakika wa kujipatia nishati kutoka Urusi itakua usoni kabisa mwa agenda ya kikao hiki-kwa muujibu wa Vladmir Shizhov,balozi wa Urusi katika UU mjini Brussels.

Kwani tangu pale ulipozuka mzozo kati ya Urusi na Ukraine juu ya nishati ya gesi hapo Januari mwaka huu pale kampuni la GAZPROM lilipofunga mfereji wa gesi kumiminika Ukraine kutokana na mabishano juu ya bei,wasi wasi ulianza kuenea juu ya uhakika wa kujipatia gesi hiyo pakizuka mutano.

UU –soko la pili kwa ukubwa duniani la nishati na ambalo laagiza hadi 20% ya mahitaji yake ya gesi kutoka Urusi,unataka uhakikishiwe kwamba mkasa ulioikumba Ucraine hautarzdiwa tena.

Kwa upande mwengine, huku UU nao ukisaka chemchem nyengine za nishati na hivyo kutia kasi mashindano masokoni, Urusi nayo inataka uhakika kwamba UU utaendelea kuagiza gesi yake mnamo muda wa kati ya miaka 10 hadi 20 ijayo.

Balaa kati ya Ucraine na Urusi juu ya gesi,liliibuka ufa uliopo katika sera ya nishati ya UU na kulibainisha wazi ushawishi mkubwa wa mali asili inavyoweza kushawishi siasa za nje.

Hali hii pia, wanadai wachambuzi inamurika imani mpya kwa Urusi chini ya rais Putin,anaekutana leo na rais wa Tume ya Ulaya Jose M anuel Barroso,msemaji wa siasa za nje wa UU Javier solana na Kanzela wolfgang Schüssel wa Austria.

Maafisa mjini Brussels wanaamini kuwa maswali ya nishati yaweza kujumuishwa katika ushirika wa mwaka ujao baina ya UU na Urusi,ulioasisiwa mwaka 1996 ambao wakati huu unajadiliwa upya.

Kwa ufupi,UU una azma katika kikao hiki kuimarisha mafungamano kati yake na Urusi ya nishati-hali ambayo ameieleza rais wa Tume Barroso ni ya manufaa tu kwa pande zote mbili.Isitoshe, makampuni ya Ulaya yanataka pia Urusi ifungue milango yake kwa ma bomba yake ya gesi na zana nyengine wakati Urusi ingependelea kufunguliwa nayo mango kueneza gesi yake katika masoko ya Ulaya.

Kamishna wa nishati wa UU Ferran Tarradellas amesema kupeana maana yake, pawepo kanuni wazi kabisa kwa makampuni ya UU kutia raslimali zao nchini Urusi na makampuni ya Urusi nayo, kutia raslimali zao katika Umoja wa ulaya.