1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G20 kumalizika India bila tamko la pamoja

18 Julai 2023

Mkutano wa siku mbili wa mataifa 20 yaliyostawi na yanayoinukia kiuchumi G20 utakamilika Jumanne huko India. Mambo kadhaa yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na vita vya Ukraine,umasikini na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

https://p.dw.com/p/4U3id
Indien | G20
Picha: Aamir Ansari/DW

Kulingana na maafisa wa India, mkutano huo wa G20 utamalizika bila taarifa ya pamoja kuhusu vita vya Ukraine kutokana na tofauti kati ya mataifa makubwa juu ya mzozo huo. Nchi za magharibi ikiwemo Marekani, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa zilishinikiza kulaani vikali uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, lakini Urusi na mshirika wake China walipinga hatua hiyo.

Wakati wa uongozi wake wa kupokezana wa G20, India ilitarajia kuleta mabadiliko kunako mageuzi ya benki za kimataifa na kutoa mwongozo wa kanuni za matumizi ya sarafu za mtandaoni na kushughulikia azimio la madeni ya nchi masikini, lakini mzozo wa Urusi na Ukraine umefifiza diplomasia ya kimataifa.

Indien Gandhinagar | vor G20-Treffen der Finanzminister | Weltbank-Chef Ajay Banga
Kiongozi mpya wa Benki ya Dunia Ajay Banga Picha: SAM PANTHAKY/AFP

Katika mkutano wa mawaziri wa fedha wa G20 huko India, Kiongozi mpya wa Benki ya Dunia aliyechukua wadhifa huo mwezi uliopita, Ajay Banga amesema hii leo kwamba tofauti zilizopo kati ya mataifa tajiri na maskini zinahatarisha kuzidisha umaskini katika ulimwengu unaojaribu kupiga hatua ya maendeleo. Banga amesema anahofia iwapo hakutokuwa mabadiliko yoyote, basi uchumi wa dunia upo hatarini kugawinyika.

Nchi nyingi bado hazijapata ahueni kutokana na pigo la janga la UVIKO-19 na athari za vita vya Urusi huko Ukraine, ambavyo kwa ujumla vimeathiri bei ya mafuta ghafi na hata bidhaa muhimu duniani kote. Wakati huo huo, nchi masikini zinakabiliwa zaidi na athari ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Mazungumzo ya G20 yanamalizika baada ya Urusi hapo jana kukataa kurefusha makubaliano ya kuruhusu usafirishaji na mauzo ya nafaka muhimu za Ukraine kupitia Bahari Nyeusi, na hivyo kuzua wasiwasi mkubwa kutoka kwa Umoja wa Mataifa, ambao wameonya kuwa mamilioni ya watu hasa kutoka mataifa maskini zaidi duniani wataathirika pakubwa.

Matarajio ya ulimwengi katika mkutano huo wa G20

Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen, amesema hapo jana kuwa ulimwengu una matumaini kwa yatakayoafikiwa katika mkutano huo:

Indien Gandhinagar | vor G20-Treffen der Finanzminister | US-Finanzministerin Yellen
Waziri wa Fedha wa Marekani Janet YellenPicha: SAM PANTHAKY/AFP

"Ulimwengu unaitazama G20 ili kuleta maendeleo katika changamoto muhimu kama vile mabadiliko ya tabianchi na magonjwa ya miripuko kama sehemu ya kazi yetu ya kuimarisha uchumi wa dunia na kuzisaidia nchi zinazoendelea. Nina matumaini tunaweza kupiga hatua madhubuti katika mikutano yetu. "

Jopo huru lililoteuliwa na kundi la mataifa ya G20 ili kutoa mapendekezo ya mageuzi kwa benki za maendeleo za kimataifa, limebaini kuwa ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu, kunahitajika karibu dola trilioni 3 kila mwaka hadi ifikapo mwaka 2030 ili kushughulikia uwekezeji unaokuwa katika suala zima la mabadiliko ya tabianchi.

Benki ya Dunia imesema inajaribu kuongeza uwezo wake wa kifedha ikiwa ni pamoja na kuongeza mitaji kutoka kwa wanahisa ili kuchochea ukuaji wa uchumi na ajira lakini ikaonya kuhusu uchafuzi wa mazingira. Mikataba ya urekebishaji wa deni kwa mataifa yenye mapato ya chini limekuwa suala kuu katika mkutano wa G20 lakini ni hatua chache tu zilizofikiwa.