Mkutano wa EU wakamilika bila muafaka wa hati za dhamana
24 Mei 2012Viongozi wengine walisisitiza umuhimu wa kupanga hafla hiyo lakini hawakutoa hatua ambazo zinaweza kuisaidia Ugiriki kusalia katika kanda hiyo. Pia suala ambalo halikushughulikiwa lilikuwa kile bara Ulaya linapaswa kufanya ili kuimarisha ukuaji wa uchumi na kurejesha imani ya wawekezaji, ambao wamesababisha gharama za ukopaji kwa nchi nyingine kufikia viwango visivyoaminika.
Mpango wa kubana matumizi ambao Ujerumani imeupigia upatu kama suluhisho kwa tatizo la Ulaya la madeni mengi ya serikali umekumbwa na ukosoaji katika nchi nyingine za sarafu ya euro.
Hati za dhamana bado suala tata
Viongozi wa nchi 27 zinazounda Umoja wa Ulaya walikubaliana kuzipa taasisi kama vile Benki ya Uwekezaji ya Ulaya jukumu la kuandaa pendekezo la ukuaji kabla ya mkutano ujao wa kilele unaopangwa mwezi Juni.
Lakini kulikuwa na ugomvi kuhusu hatua zaidi kali zinazoshinikizwa na baadhi ya viongozi wanaohudhuria kikao hicho, kama vile kutoa hati dhamana kwa pamoja kama njia moja ya kupunguza gharama za kukopa kwa mataifa yaliyo na madeni makubwa miongoni mwa nchi 17 zinazotumia sarafu ya euro.
Dhana kuwa viongozi wa Ulaya wanakosa nia ya kisiasa ya kuyakabili matatizo ya kifedha na kiuchumi barani humo imeyafanya masoko ya fedha kuyumba katika wiki kadha azilizopita. Mdororo wa kiuchumi unasambaa. Benki ziko chini ya shinikizo. Wasiwasi ni kuwa ikiwa Ugiriki haitaokolewa, mataifa mengine kama vile Ureno na Uhispania huenda yakatumbukia katika tatizo kama hilo. Waziri Mkuu wa Luxembourg Jean-Claude Juncker anasema nchi za sarafu ya euro ni sharti zizingatie aina yote ya matukio, lakini akasisitiza kuwa wazo lililopo kwa sasa ni kuwa Ugiriki itasalia katika ukanda wa sarafu ya euro. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema baada ya mkutano huo kuwa wanataka Ugiriki isalie katika kanda ya euro.
Ugiriki yapigiwa upatu
Lakini mkutano huo wa leo wa viongozi wa EU umekamilika bila makubaliano yoyote.
Taarifa ya mwisho ilisema Ugiriki ni sharti iheshimu ahadi zake na ikatilia mkazo fedha ambazo kanda ya euro na shirika la fedha la Kimataifa IMF yaliikopesha Ugiriki kama ishara ya wao kuonyesha mshikamano.
Ilisema kuwa fedha za maendeleo ya uchumi zitatumwa kwa Ugiriki. Rais wa Ufaransa Francois Hollande alisema hali hiyo inaweza kutuma ujumbe kwa masoko kuwa ukanda wa euro haushirikiani na Ugiriki.
Viongozi pia waliangazia suala tata la ikiwa nchi zinazotumia sarafu ya euro zinafaa kujweka hatarini na kukopa pesa kwa pamoja, kwa kutoa kile kinachojulikana kama hati dhamana za sarafu ya euro. Hii ina maana kuwa kila nchi huenda ikakopafedha kwa kiwango sawa, na kupunguza gharama za zile nchi zilizo na madeni. Hollande ameshinikiza suala hilo kama njia moja ya kuhakikisha kuwa mzozo kama huo hautokei tena, lakini Merkel amekataa, akihofia kuwa zinaweza kupunguza shinikizo dhidi ya serikali zilizo na madeni makubwa sana kuokoa fedha zao na kuilazimisha Ujerumani kukopa kwa viwango vya juu
Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Sekione Kitojo