1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Baraza Kuu la UN wafunguliwa New York

18 Septemba 2023

Viongozi wa mataifa mbalimbali wanaoendelea kuwasili nchini Marekani wanakabiliwa na shinikizo la kutafutia suluhu ifikapo mwaka 2030, masuala muhimu ikiwa ni pamoja na kukabiliana na migogoro.

https://p.dw.com/p/4WTn5
Malengo ya maendeleo endelevu yajadiliwa NewYork
Malengo ya maendeleo endelevu yajadiliwa NewYorkPicha: Mike Segar/REUTERS

Mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umefunguliwa rasmi hii leo jijini New York. Viongozi wa mataifa mbalimbali wanaoendelea kuwasili nchini Marekani wanakabiliwa na shinikizo la kutafutia suluhu ifikapo mwaka 2030, masuala muhimu ikiwa ni pamoja na kukabiliana na migogoro, umasikini, njaa, elimu bora, usawa wa kijinsia pamoja na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anajaribu kuanzisha hatua za kufikia malengo 17 muhimu ya maendeleo endelevu yenye lengo la kuziba pengo linaloongezeka la ukosefu wa usawa kati ya mataifa tajiri na maskini.

Guterres amesema malengo hayo yana dhamira ya kurekebisha makosa ya kihistoria na kupunguza hali ya migawanyiko duniani.

"Nyote ni sehemu ya juhudi kubwa za kimataifa kuokoa malengo hayo muhimu ya maendeleo endelevu, na mnapaswa kuchukua hatua zinazotegemewa na sayari yetu pamoja na watu ulimwenguni kote.", alisema Guterres.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, ikiwa mambo yatasalia kama yalivyo, watu milioni 575 watakuwa wanaishi katika umaskini mkubwa na zaidi ya wengine milioni 600 watakabiliwa na njaa ifikapo mwaka 2030.