1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuhusu Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini

Sylvia Mwehozi
6 Aprili 2019

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kwamba kuna haja kuitazama Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini sio kwasababu ya maeneo yaliyo na migogoro bali pia kama ukanda ulio na fursa.

https://p.dw.com/p/3GP21
Jordanien World Economic Forum on the Middle East and North Africa 2019
Picha: Reuters/M. Hamed

Guterres ametoa kauli hiyo katika ufunguzi wa Kongamano la Uchumi Duniani (WEF), kuhusu Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini linalofanyika nchini Jordan. Aidha amesifu nchi kadhaa namna zilivyoweza kujumuisha katika katiba zao baadhi ya mahitaji ya kisiasa yanayoelezewa mitaani na kuimarisha ulinzi wa kijamii, utawala bora na haki za binadamu.

Mwaka 2011, vuguvugu la maandamano lilienea katika ukanda wa nchi za kiarabu wakati vijana waliposhinikiza juu ya mageuzi na kuwaondoa watawala wa muda mrefu. Baadhi ya vuguguvu liligeuka kuwa migogoro ya muda mrefu ikiwemo nchini Syria, Libya na Yemen.

Guterres pia amegusia hatari ya mabadiliko ya tabia nchi. "Ukanda huu utakabiliana na athari kubwa hususan ongezeko la ukosefu wa maji, ambao utapunguza kiwango kilichopo cha ardhi na kuongeza utegemezi wa chakula kutoka nje", alisema Guterres.

Jordanien World Economic Forum on the Middle East and North Africa 2019 | King Abdullah und Abdullah Abdullah
Mfalme Abdullah wa Jordan na mkurugenzi wa Afghanistan Abdullah AbdullahPicha: Reuters/M. Hamed

"Nchi kama Jordan ambayo haichangii sana katika mabadiliko ya tabia nchi haiwezi kuwa mwathirika kutokana na hoja kwamba baadhi ya nchi hazitimizi wajibu wake".

Awali wakati akifungua kongamano hilo Mfalme Abdullah wa Jordan ametoa wito wa uwekezaji zaidi wa kigeni katika Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini, akisema uwekezaji huo unahitajika ili kutengeneza "mustakabali wa baadae" wa ukanda huo uliokumbwa na migogoro.

"Hali yetu ya kiuchumi inatia moyo", alisema Abdullah, lakini akiongeza kuwa uchumi wa Jordan umekabiliwa na changamoto nyingi wakati taifa hilo "lilipofanya jambo sahihi kushughulikia wakimbizi". Jordan inawahudumia wakimbizi karibu milioni 1.3 kutoka Syria.

Ili kufufua uchumi wake, serikali ilichukua hatua kadhaa za kubana matumizi katika siku za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kupunguza ruzuku katika bidhaa za msingi kama vile mkate, ili kufufua uchumi na kupunguza pengo la upungufu wa bajeti.

"Mageuzi yako mbioni ili kuunga mkono na kuboresha mazingira ya biashara", alisema Mfalme huyo katika kongamano linalofanyika karibu na bahari iliyokufa yaani Dead Sea.

Naye waziri wa mambo ya nje wa Oman Yusuf bin Alawi bin Abdullah amesema nchi za Kiarabu zinapaswa kukomesha hofu kuhusu uwepo wa Israel. Mnamo Israel ikipokea uungwaji mkono wa kisiasa, kiuchumi na kijeshi kutoka jumuiya ya kimataifa, bado ina wasiwasi juu ya hatma yake kama nchi isiyo mwanachama wa mataifa ya kiarabu katika ukanda.

Jordanien World Economic Forum on the Middle East and North Africa 2019
Mfalme Abdullah wa Jordan Picha: Reuters/M. Hamed

"Inahisi kutokuwa salama katika ukanda huu na nafikiri nchi za kiarabu zinapaswa kulitazama hili na kukomesha wasiwasi huo", alisema waziri huyo katika kongamano la siku mbili nchini Jordan.

Kauli ya waziri huyo wa Oman inakuja katikati mwa juhudi za kurejsha uhusiano baina ya Oman na Israel baada ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu kutembelea taifa hilo mwezi Novemba na kukutana na Sultan Qaboos Bin Said.

Hata hivyo kauli yake imepingwa na waziri mwenzie wa Jordan Ayman al-Safadi, ambaye alisema tatizo ni kukataa kwa Israel kuondoka katika maeneo iliyoyatwaa tangu mwaka 1967 na kuruhusu uanzishwaji wa taifa la Palestina.

"Jumuiya ya Kiarabu imetambua haki ya uwepo wa Israel, Wapalestina wenyewe wametambua haki ya uwepo wa Israel, tatizo lililopo ni kukaliwa kwa maeneo, je kukaliwa huko kutaisha au", alisema waziri huyo wa Jordan na kupigiwa makofi na washiriki wa kongamano.

Kongamano hilo la siku mbili, linajadili ukosefu wa ajira, migogoro, maendeleo ya kiuchumi na mabadiliko ya tabianchi katika maeneo hayo. Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov wote wanahudhuria kongamano hilo linalohudhuriwa na wajumbe wapatao 1000.

Mkutano huo umefanyika wakati kunafanyika machafuko ya kijeshi nchini Libya, pamoja na vuguvugu la kudai demokrasia nchini Algeria lilomlazimisha Rais Abdelaziz Bouteflika kung'oka madarakani baada ya kuiongoza nchi hiyo kwa miaka 20.