1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutan wa kilele.

Mtullya, Abdu Said14 Novemba 2008

Urusi na Umoja wa Ulaya zitaanza tena mazungumzo juu ya ushirikiano.

https://p.dw.com/p/Fuye
Marais Sarkozy wa Ufaransa na Medvedev wa Urusi baada ya mkutano wao mjini Nice leo.Picha: AP

Rais Nicolas Sarkozy wa  Ufaransa anaeuongoza Umoja  wa Ulaya kwa sasa ameitaka Urusi ikubali kufanya mazungumzo juu  ya usalama  wa Ulaya kabla ya kuweka makombora karibu na mipaka ya nchi za Ulaya  magharibi. 

Rais Sarkozy amesema hayo leo mjini Nice  baada  ya mkutano baina  ya viongozi wa Umoja  wa Ulaya na Urusi.

Akizungumza  kwenye  mkutano  na wandishi  habari katika  wa Nice nchini Ufaransa rais  Sarkozy  alisema kuwa rais Dmitry Medvedev  wa Urusi ametoa mwitikio mzuri juu ya pendekezo hilo.

Rais Sarkozy wa Ufaransa anaeuongoza   Umoja  wa Ulaya kwa sasa  amefahamisha  kuwa mazungumzo hayo yanaweza kufanyika kati kati ya mwaka ujao.

Marais hao walizungumza na wandishi habari  baada ya mkutano  baina ya viongozi wa Umoja   wa Ulaya na Urusi ambapo  pande mbili hizo zilijadili masuala ya ushirikiano,usalama na mgogoro wa fedha.

Wiki iliyopita Urusi ilitangaza kuwa itaweka  makombora Kaliningrad ili kukabili inachoita kuwa ni hatari inayotokana  na uamuzi wa Marekani juu ya  kuweka makombora ya  kujihami nchini Poland na katika jamhuri ya Chek.

Hatahivyo rais Dmitry Medvedev amezitaka  nchi za Ulaya magharibi  ziwe na subira juu ya   suala hilo. Amezitaka nchi hizo ziepuke kuchukua hatua  za upande mmoja kabla ya  kufikiwa makubaliano juu  ya kuweka msingi  wa usalama barani Ulaya.

Juu ya uhusiano  baina ya Urusi  na nchi za  Umoja  wa  Ulaya  rais wa  tume ya Umoja huo Jose Manuel Barosso amefahamisha  kuwa  mazungumzo juu ya ushirikiano  kati   ya pande   mbili hizo yataanza tena baada ya   kusimamishwa hivi karibuni kutokana na vita  baina ya Urusi na Georgia.

Mazungumzo hayo yalianzishwa mwaka jana  kwa lengo la kuleta ushirikiano mkubwa zaidi katika sekta  za uchumi,usalama na sheria.


Kwenye mkutano wao mjini Nice rais Sarkozy   wa Ufaransa  mwenzake wa Urusi Medvedev  pia walijadili mgogoro wa fedha ulioikumba  dunia.

Viongozi  hao wametoa mwito juu ya kuleta  mageuzi makubwa katika taasisi muhimu za  fedha duniani. Rais Medvedev ameilaumu Marekani kwa mgogoro huo wa  fedha  na amesema kuwa  nchi yake  inataka  mabadiliko yafanyike katika taratibu  zinazotumika kwenye  taasisi za fedha ili kuweza kupunguza  usemi mkubwa  wa nchi za magharibi kwenye taasisi  hizo.

Marais Sarkozy wa Ufaransa na Medvedev wa Urusi  wanatarajiwa kuwasili mjini Washington kuhudhuria mkutano wa  nchi 20, utakaofanyika kesho ,kujadili msukosuko ulioyakumbuka masoko ya fedha duniani.