1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkakati wa Urusi kutuma silaha Afrika

4 Juni 2020

Sambamba na maliasili, mauzo ya nje ya silaha ni vipengele muhimu vya uchumi wa Urusi. Katika miongo miwili iliyyopita, Urusi imeweza kuimarisha uhusiano wake na Afrika na kugeuka muuzaji mkubwa wa silaha barani humo.

https://p.dw.com/p/3dG98
Silaha kutoka Urusi
Picha: picture-alliance/Newscom/R. Ben Ari

Kampuni ya uuzaji silaha ya serikali ya Urusi Rosoboronexport ilitangaza mnamo mwezi Aprili, mkataba wake wa kwanza wa mauzo ya boti za mashambulizi kwa taifa la kanda ya Afrika kusini mwa Sahara. Lakini jina la taifa hilo liliwekwa kapuni. Kinachofahamika ni kwamba: Huo ndiyo ulikuwa mkataba wa kwanza wa mauzo ya nje ya bidhaa za kwanza jeshi la majini zilizotengenenzwa nchini Urusi kwa eneo hili katika muda wa miaka 20 iliyopita.

Ingawa habari hii haikuvutia sana nadharia ya kimataifa, mkataba huu mpya unaimarisha njia ya Urusi kukita mizizi barani Afrika na kupanua ramani yake ya mauzo ya nje ya silaha barani humo. Jukumu la Urusi barani Afrika, ambayo iliwahi kuwa muuzaji mkuu katika enzi za Jamhuri ya Kisovieti, lilipungua baada ya kuporomoka kwa jamhuri hiyo ya kisovieti.

Taarifa zaidi: Umoja wa Mataifa wathibitisha mamluki wa Urusi wanapigana Libya

Lakini kufikia mwaka 2000, Urusi ilianza kupenyeza tena, na katika kipindi cha miongo miwili, imeweza kuwa muuzaji mkubwa zaidi wa silaha barani Afrika. Kwa sasa inachangia asilimia 49 ya mauzo ya silaha barani Afrika, kwa mujibu wa kanzudata ya taasisi ya kimataifa ya utafiti wa amani SIPRI, yenye makao yake mjini Stockholm, nchini Sweden.

Je mgogoro wa Libya wageuka kuwa wa Mataifa ya nje?

Tangu mwaka 2000, mauzo ya silaha ya Urusi kwa mataifa ya Afrika yameongezeka pakubwa. Ongezeko hilo limetokana hasa na kukua kwa mauzo ya silaha za Urusi kwa taifa la Algeria, ambayo mpaka sasa inasalia kuwa mnunuzi mkubwa zaidi wa silaha za Urusi barani, ikifuatiwa na Misri, Sudan na Angola.

Urusi yataka kufaidika na mizozo ya Afrika

Kwa mujibu wa Alexandra Kuimova, mtafiti katika programu ya matumizi ya silaha na kijeshi ya SIPRI, idadi ya mataifa ya Afrika yanayonunua silaha za Urusi imeongezeka katika kipindi cha miongo miwili iliyopita. Mwanzoni mwa 2000, mataifa 16 ya Afrika yalikuwa yakipokea silaha za Urusi. Kati ya 2010 na 2019, idadi hiyo imeongezeka hadi 21.

Kuongezeka kwa shauku ya Urusi barani Afrika kunafasiriwa siyo tu kiuchumi, bali pia na sababu za kisiasa na kimkakati. Urusi inaitazama Afrika kama mshirika muhimu katika dira ya utaratibu wa dunia wenye ncha nyingi tofauti. Wakati wa mkutano wa kwanza wa kilele kati ya Urusi na Afrika mjini Sochi mwaka 2019, Rais Vladmir Putin, alisema kuimarishwa kwa uhusiano na mataifa ya Afrika ni moja ya vipaumbele vya sera ya kigeni ya Urusi.

Rais Vladimir Putin katika mkutano wa kilele na viongozi wa Afrika
Rais Vladimir Putin katika mkutano wa kilele na viongozi wa Afrika Picha: picture-alliance/dpa/Pool/Tass/V. Sharifulin

Lakini katika nyaraka za kimkakati za Urusi zinazopatikana hadharani, kama vile dhana ya sera ya kigeni au kanuni ya ulinzi, mataifa ya Afrika yanaelezwa kama yaliyo kwenye bara lisilo na utulivu na yanayotoa kitisho cha kimataifa katika muktadha wa shughuli za makundi ya kigaidi, hasa katika kanda ya Afrika Kaskazini. Nyaraka kama hizo zinamulika malengo ya Urusi ya kupanua maingiliano na Afrika kwa kujenga biashara yenya faida na uhusiano wa kiuchumi na kusaidia juhudi za kikanda kuzuwia mizozo.

Ukosefu huu wa utulivu unaoendelea unahudumia soko endelevu la silaha - na kwa Urusi, Afrika inawakilisha soko muhimu bila kikomo kwa kuzingatia vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa na mataifa ya magharibi baada ya kulitwaa eneo la Crimea. Afrika ni bara ambako Urusi inaweza kuimarisha mauzo yake ya nje ya silaha, ambayo yanachangia asilimia 39 ya mapato ya sekta ya ulinzi ya taifa hilo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/DW (https://www.dw.com/en/russian-arms-exports-to-africa-moscows-long-term-strategy/a-53596471)

Mhariri: Josephat Charo