1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN : Waharibifu wanajaribu kuzuia uchaguzi nchini Libya

16 Julai 2021

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Libya Jan Kubis amewashtumu watu wanaojaribu kuzuia kufanyika kwa uchaguzi muhimu nchini Libya uliopangiwa mwezi Desemba unaolenga kuliunganisha taifa hilo

https://p.dw.com/p/3wZpH
USA UN Sonderbeauftragter für den Libanon Jan Kubis
Picha: picture-alliance/Photoshot/L. Muzi

Kubis amekiambia kikao cha mawaziri wa baraza hilo kwamba amezungumza na wadau wengi wakati wa ziara yake iliyokamilika hivi karibuni nchini Libya na wote wakasisitiza kujitolea kwao kwa uchaguzi huo wa rais na ubunge wa Desemba 24 lakini akaongeza kuwa ana hofu wengi wao hawako tayari kuchukuwa hatua zinazohitajika. Kubis alitaja kushindwa kwa baraza la mazungumzo ya siasa za Libya lenye wanachama 75 kutoka matabaka mbali mbali kukubaliana kuhusu mfumo wa kisheria wa kuandaa uchaguzi mapema mwezi huu na kutoa mwelekeo wa kumaliza mvutano ambao umedumu kwa muongo mmoja katika taifa hilo.

Kubis aliwahimiza wanachama wa baraza hilo kuweka kando tofauti zao na kukubaliana kuhusu pendekezo la msingi wa kikatiba wa uchaguzi ambao baraza la wawakilishi linaweza kuidhinisha mara moja. Taarifa ya rais iliyoidhinishwa na baraza la usalama iliunga mkono wito wa Kubis wa hatua za haraka na sheria ya kuiruhusu tume ya kitaifa ya uchaguzi nchini humo kuwa na muda wa kutosha na raslimali za kujiandaa kwa uchaguzi.

vikwazo vya Umoja wa Ulaya

Baraza hilo lilisisitiza kuwa watu binafsi na makundi yanaweza kuwekewa vikwazo vya kifedha na usafiri iwapo kamati ya baraza hilo inayofuatilia utekelezwaji wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa itathibitisha kuwa wanahusika ama kuunga mkono vitendo vinavyotishia amani, uthabiti ama usalama nchini Libya ama pia kuhujumu mchakato wa mpito wa kisiasa nchini humo na kusisitiza kuwa vitendo kama hivyo huenda vikazuia ama kuhujumu chaguzi zilizopangwa katika mipango ya baraza hilo. Baraza hilo la usalama pia liliyahimiza mataifa yote, pande husika nchini Libya na wadau wengine husika kutekeleza kikamilifu makubaliano ya kusitisha mapigano yanayojumuisha kuondoka kwa vikosi vya kigeni na mamluki kutoka Libya mara moja.

Mkutano wa baraza hilo la usalama unafuata kongamano la mwezi uliopita kuhusu Libya mjini Berlin nchini Ujerumani ambapo Ujerumani na Umoja wa Mataifa iliyaleta pamoja mataifa 17 na uongozi wa mpito nchini Libya kushinikiza utekelezwaji wa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano na mwelekeo wa uchaguzi. Taarifa hiyo ya rais ilipongeza yalioafikiwa katika kongamano hilo.