1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yashutumiwa kwa kuwakamata wanaharakati na wakosoaji

26 Juni 2020

Waandishi kadhaa wa habari pamoja na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Misri wamekamatwa kufuatia kampeni mpya inayowalenga wale wanaoikosoa serikali.

https://p.dw.com/p/3eP0f
Deutschland Compact with Africa Initiative in Berlin | Agyptischer Präsident al-Sissi
Picha: picture-alliance/AFP/J. Macdougall

Maafisa wa kutetea haki za binadamu wameshutumu hatua hiyo ya Misri na wamezitaka Ujerumani pamoja na Umoja wa Ulaya kuchukua hatua muafaka.

Mnamo siku ya Jumatano, Nora Younis ambaye ni mhariri mkuu wa tovuti kwa jina al-Manassa inayojishughulisha na usambazaji habari alikamatwa na kushikiliwa rumande baadaye alishtakiwa kwa kosa la kuisimamia tovuti hiyo ya habari bila leseni. Tovuti yake imesema kuwa, Younis aliachiliwa kwa dhamana siku ya Alhamisi jioni baada ya mahojiano ya muda mrefu.

Msako katika ofisi za Al-Manassa

Katika tukio hilo, maafisa waliwakamata jumla ya watu wanane baada ya kufanya msako kwenye ofisi ya tovuti hiyo binafsi na kufanya upekuzi ikiwemo kwenye tarakilishi.

Mnamo mwezi uliopita, maafisa wa Misri waliwakamata wanaharakati kadhaa kwa makosa ambayo wanaharakati wanahoji ni ya kubabikiziwa, ikiwa ni pamoja na kuchochea ugaidi, kueneza habari za uongo na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii. Wameongeza kuwa serikali ya Misri inaona kuwa muda umewadia wa kuwanyamazisha wakosoaji wake.

Nora Younis ambaye ni mhariri wa tovuti ya habari ya Al-Manassa alikamatwa baada ya msako w apolisi katika ofisi ya tovuti hiyo.
Nora Younis ambaye ni mhariri wa tovuti ya habari ya Al-Manassa alikamatwa baada ya msako w apolisi katika ofisi ya tovuti hiyo.Picha: Al-Manassa/Twitter

Wengine ambao wamekamatwa tangu mwezi uliopita ni pamoja na Mohamed Mounir, Sanaa Seif na jamaa za mwanaharakati aliyeko Marekani Mohammed Soltan.

HRW: Janga la COVID-19 limefanya masuala ya kimataifa kusahauliwa

Amr Magdi ambaye ni mtafiti wa shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch nchini Misri, amesema kuwa kufuatia janga la corona, serikali za magharibi zinashughulikia tu masuala ya ndani ya nchi zao badala ya kufuatilia pia ukiukaji wa haki za binadamu kimataifa, hali ambayo imeiruhusu serikali ya rais wa Misri Abdel Fattah el-Sissi kuendeleza ukandamizaji.

Magdi ameongeza kuwa asasi za usalama nchini Misri zinafahamu kuwa Wamisri wameghadhabishwa na maandamano yanaweza kutokea, hivyo zinajaribu kuzuia ukosoaji wowote usitokee.

Kwa mujibu wa Magdi, Ujerumani, Umoja wa Ulaya na Marekani zina wajibu wa kushutumu mashambulizi ya kiholela dhidi ya haki za binadamu nchini Misri.

Wanaharakati ni miongoni mwa wale ambao serikali ya Misri inatuhumiwa kujaribu kunyamazisha sauti na ukosoaji wao. Kwenye picha hii ya maktaba Agosti 28, 2014 ni mwanablogu maarufu Alaa Abdel-Fattah (kushoto) na dadake Sanaa Abdel-Fattah.
Wanaharakati ni miongoni mwa wale ambao serikali ya Misri inatuhumiwa kujaribu kunyamazisha sauti na ukosoaji wao. Kwenye picha hii ya maktaba Agosti 28, 2014 ni mwanablogu maarufu Alaa Abdel-Fattah (kushoto) na dadake Sanaa Abdel-Fattah.Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Ammar

Hofu ya kutokea maandamano dhidi ya serikali Misri

Maafisa wa serikali wanaonekana kuzidi kuwa na wasiwasi juu ya jinsi masuala tete yanavyoangaziwa hadharani na vyombo vya habari. Wiki iliyopita, baraza la vyombo vya habari nchini humo lilionya kuwa shirika lolote linaloripoti bila kufuata utaratibu wa serikali kuhusu janga la COVID-19, mzozo wa Libya, wa Sinai au kuhusu mvutano na Ethiopia kuhusu bwawa katika mto Nile.

Awali, tovuti ya al-Manassa, iliripoti kuwa ilituma ombi la kupewa leseni mnamo mwaka 2018 lakini halikupata jibu.

Sayyid Turki ambaye ni mhariri mwandamizi wa tovuti ya Al-Manassa amesema wimbi la ukamataji imekuwa hali ya kawaida kwa sasa nchini Misri. Ameongeza kuwa hatua ya tovuti hiyo kuangazia kile kinachotajwa kuwa ‘hali yenye utata kuhusu COVID-19' huenda imechangia kukamatwa kwa Younis.

Al-Manassa, ni miongoni mwa tovuti ambazo zimepigwa marufuku nchini Misri tangu mwaka 2017.

Vyanzo: APE, DW