1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yapata ushindi wa kwanza AFCON

16 Januari 2022

Mohamed Salah apachika wavuni bao ya ushindi la timu ya taifa ya Misri siku ya Jumamosi dhidi ya Guinea-Bissau baada ya Nigeria kufuzu kwa hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

https://p.dw.com/p/45azR
Fußball | Africa Cup of Nations | Guinea Bissau - Ägypten
Picha: AP Photo/Footografiia/picture alliance

Kunako dakika ya 69 ya mchezo Salah alitia kimyani bao la pekee na la ushindi kwa mabingwa mara saba wa kombe hilo, Misri, na kuimarisha kampeni zao za kuwania ubigwa baada ya kulazwa na Nigeria bao 1-0 katika mchezo wao wa ufunguzi kwenye Kundi D.

soma Macho yaelekezwa kwa Afcon Cameroon

Guinea-Bissau walikasirika baada ya bao maridadai kutoka kwa mchezaji wao Mama Balde kunako dakika ya 82 kufutwa kufuatia uhakiki wa VAR.

Kocha wa Misri Carlos Queiroz na kikosi chake sasa wanahitaji angalau sare katika mechi yao ya mwisho dhidi ya majirani zao Sudan siku ya Jumatano ili kufuzu kwa raundi ya 16 bora.

"Ulikuwa mchezo mgumu sana na tulikuwa na bahati ya kupata ikabu, lazima tushinde mchezo wetu unaofuata sasa ili kuhakikisha tunafuzu na tutajitahidi kadri tuwezavyo katika michuano hii" Salah alikiri kwa watangazaji.

soma Ivory Coast yapata ushindi dhidi ya Guinea ya Ikweta

Salah,  hakuwa amefunga katika mechi sita zilizopita alizocheza Misri msimu huu. Nyota mshambuliaji wa klabu ya Uingereza Liverpool ameondoa udhia baada kupokea pasi kutoka kwa Amr El Solia na kufyatua mkwaju uliomuacha mlinda lango wa Guinea-Bissau Jonas Mendes akiduwaa.

Guinea-Bissau taifa dogo la Afrika Magharibi wamefuzu kwa mechi za AFCON mara tatu mfululizo lakini bado wanaendelea kutafuta ushindi wao wa kwanza kwenye michuano hiyo.

Nigeria yafuzu kwa mchujo wa 16 bora

Fußball Africa Cup of Nations | Nigeria vs Ägypten
Wachezaji wa NigeriaPicha: Samuel Shivambu/BackpagePix/picture alliance

Nigeria inayoongoza katika bara la Afrika ilifuzu kwa awamu ya muondoano baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya Sudan katika uwanja wa Roumdé Adjia kaskazini mwa Cameroon.

Nyota wa zamani wa Super Eagles, Augustine Eguavoen akihudumu kama kocha wa muda baada ya kutimuliwa kwa kocha Mjerumani Gernot Rohr,mwezi uliopita.  Nigeria ilitumia kikosi kile kile kilichoifunga bao 1-0 Misri.

Mabao ya Nigeria yalitiwa kimyani na Samuel Chukwueze anasakata soka katika klabu ya Villarreal dakika ya tatu, bao la pili Taiwo Awoniyi dakika ya 45 na Moses Simon akafunga la tatu dakika ya 46 ya mchezo.

Bao la pekee la Sudan lilifungwa na mchezaji Walieldin Khidir kunako dakika ya 70. 

Mechi nyengine

Fussball - 2021 Africa Cup of Nations - Kamerun
Picha: Alain Guy Suffo/empics/picture alliance

Siku ya Jumapili (16.01.2022) mabingwa watetezi Algeria wanatafuta ushindi wao wa kwanza watakapocheza na Equatorial Guinea mjini Douala baada ya Ivory Coast kumenyana na Sierra Leone katika kundi E.

Tunisia ambayo imekosa wachezaji wengi kutokana na kupatikana na virusi vya corona itakabiliana na Mauritania katika mji wa Limbe ulioko pwani huku  Gambia ikitarajiwa kumenyana na Mali katika uwanja huo huo.

Mshambulizi wa Ghana Benjamin Tetteh amepigwa marufuku ya mechi tatu baada ya kumpiga ngumi mchezaji wa Gabon wakati wa rabsha kubwa mwishoni mwa mchezo wa Ijumaa uliomalizika kwa sare ya 1-1 dhidi ya Gabon.

Marufuku hiyo ina maana kwamba hataweza kucheza tena kwenye michuano hiyo isipokuwa Ghana itakapofuzu kwa nusu fainali.

 

Samuel Eto'o atafuta sifa ndani na nje ya uwanja

 

AFP