Misaada yashindwa kufikishwa maeneo ya mafuriko Afghanistan
12 Mei 2024Katika eneo la Sheikh Jalal, mojawapo ya maeneo yaliyoharibiwa zaidi, AFP imeelezea kuhusu malori ya misaada yaliojaa chakula, magari ya kijeshi, maafisa wa uokoaji na wakaazi wa eneo hilo wakiwa wamekwama katika maeneo ambayo barabara zilikuwa zimesombwa kabisa.
Soma pia:WFP: Mvua imesababisha vifo vya watu 300 Afghanistan
Mohammad Ali Aryanfar, mmoja wa maafisa wa shirika la Uturuki la kutoa msaada wa kibinadamu la Hak linalojaribu kupeleka chakula katika eneo la Burka, amesema wamekuwa barabarani tangu mapema leo lakini wamekwama katika eneo la Sheikh Jalal.
WFP yatumia njia mbadala kufikisha msaada katika maeneo yalioathirika
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani - WFP, lilituma picha kwenye mtandao wa kijamii wa X likionesha mifuko ya unga ikiwa imefungwa kwenye migongo ya punda, na kusema iliwabidi kutafuta njia mbadala ili kufikisha chakula hicho kwa manusura wa mafuriko hayo huko Baghlan.