1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miripuko miwili yaitikisa Kampala

16 Novemba 2021

 Miripuko miwili katika mji mkuu wa Uganda, Kampala, inakhofiwa kuwajeruhi watu kadhaa katika kile polisi wanachosema ni "mashambulizi" dhidi ya mji huo wenye shughuli nyingi na ikiwa mara ya nne ndani ya mwezi mmoja.

https://p.dw.com/p/433Me
Uganda I Explosion in Kampala
Picha: Hajarah Nalwadda/XinHua/picture alliance

"Tunachoweza kusema ni kwamba haya ni mashambulizi lakini kuhusiana na aliyehusika, hilo bado ni suala linalochunguzwa," Naibu Mkuu wa Polisi ya Uganda, Edward Ochom, aliliambia shirika la habari la AFP.

"Miripuko ilitokea karibu na Kituo Kikuu cha Polisi na mengine karibu na lango la Bunge, maeneo yote yapo katikati ya eneo la kibiashara," alisema, akiongeza kwamba majeruhi wamepelekwa hospitalini.

Mripuko uliotokea karibu na kituo cha polisi ulivunja vioo vya madirisha wakati ule wa karibu na lango la bunge ukizisababisha gari kadhaa zilizoegeshwa hapo kuunguwa moto, kwa mujibu wa polisi.

"Tumetuma timu ya uokozi kwenye eneo hilo," alisema msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Uganda, Irene Nkasiita.

Kyle Spencer, ambaye ni mkurugenzi mkuu wa Internet Exchange Point nchini Uganda na ambaye aliisikia miripuko hiyo, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba watu walipata mshituko na wasiwasi mkubwa kutokana na miripuko hiyo.

Uganda | Polizeiwagen | Festnahme Francis Zaake
Gari la polisi mjini Kampala katika operesheni ya usalama.Picha: Luke Dray/Getty Images

"Barabara ya kuelekea bungeni imefungwa, watu wanalia tu, kila mtu anajaribu kuyakimbia maeneo haya. Kila mtu anayakimbia majengo ya ofisi yake na majengo yamefungwa na hawaruhusu watu kuingia ndani." Alisema mkurugenzi huyo.

Bunge laakhirisha vikao

Bunge liliakhirisha kikao chake cha siku ya Jumanne kufuatia mashambulizi hayo, likiwataka wajumbe kuepuka kufika eneo hilo "wakati vikosi vya ulinzi vinapambana kurejesha usalama."

Mashambulizi hayo yanafuatia miripuko miwili mwezi uliopita, mmoja kwenye basi karibu na Kampala ambao uliwajeruhi watu kadhaa na mwengine wa bomu katika mkahawa wa njiani uliomuua mtu mmoja. 

Polisi ilisema kuwa mashambulizi yote mawili yalifanywa na kundi la waasi la Allied Democratic Forces (ADF), huku ikionya kuwa wapiganaji wa itikadi kali walikuwa wakipanga mashambulizi mengine makubwa.

ADF, ambalo kimsingi ni kundi la waasi wa Uganda, limekuwa likituhumiwa kwa mauaji ya maelfu ya raia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. 

Mnamo mwezi Machi, Marekani ililiunganisha kundi hilo rasmi na lile lijiitalo Dola la Kiislamu.