1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUgiriki

Mioto iliyokuwa ikiwaka Ugiriki imedhibitiwa

26 Julai 2023

Mioto iliyokuwa ikiwaka kwenye sehemu mbalimbali za Ugiriki imedhibitiwa leo hii Jumatano, hayo ni kulingana na taarifa za vyombo vya habari vya Ugiriki.

https://p.dw.com/p/4UQcY
Tödliche Waldbrände am Mittelmeer
Picha: Nicolas Economou/Reuters

Idara inayosimamia maswala ya hali ya hewa nchini humo imesema hali bado ni ya wasiwasi kutokana na kuwepo viwango vya juu vya joto vinavyofikia nyuzi joto 47 katika kipimo cha Celsius. Msemaji wa kikosi cha taifa cha zima moto ameiambia redio ya serikali kwamba takriban mikasa 500 ya moto wa nyikani imetokea kote nchini Ugiriki tangu Julai 12.

Kijiji maarufu cha mapumziko cha Gennadi chaokolewa

Katika saa chache zilizopita, kikosi cha zima moto cha Ugiriki na maelfu ya wasaidizi waliweza kukiokoa kijiji maarufu cha mapumziko cha Gennadi, kusini-mashariki mwa kisiwa cha Rhodes. Kwenye kisiwa cha Corfu cha kaskazini-magharibi mwa Ugiriki kuna maeneo machache ambayo bado yanateketeka lakini sio kwa kiwango kikubwa. Tume ya Umoja wa Ulaya imesema nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinashikamana na Ugiriki na zimewapeleka karibu wazima moto 500 na ndege saba kwenye maeneo mbalimbali katika juhudi za kuzima mioto iliyosambaa.