1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Mikopo ya China kwa Afrika yapungua mwaka 2022

19 Septemba 2023

Takwimu mpya zilizochapishwa leo zinaonesha kiwango cha mikopo ya China kwa mataifa Afrika kimeanguka hadi chini ya dola bilioni 1 mwaka uliopita, rikodi ambayo ni ndogo kabisa ndani ya kipindi cha karibu muongo mmoja.

https://p.dw.com/p/4WUl1
Reli ya SGR nchini Kenya
Mradi kama wa reli ya kisasa ya SGR nchini Kenya ulijengwa kwa mkopo wa ChinaPicha: Wang Guansen/Xinhua/IMAGO

Kulingana na takwimu hizo zilizokusanywa na Chuo Kikuu cha Boston, China ilitia saini mikopo yenye thamani ya dola milioni 994 pekee mwaka jana ikilinganishwa na mikopo ya dola bilioni 1.22 iliyotolewa mwaka 2021.

Kuanguka huko kwa thamani ya mikopo kunaashiria kuwa China inaachana na mwenendo wake wa miongo kadhaa wa kumwaga mabilioni ya dola barani Afrika hususani kufadhili miradi ya miundombinu.

Kwa karibu miaka kumi iliyopita Beijing iliandamwa na ukosoaji kuwa imedhamiria "kuyateka nyara" mataifa mengi yanayoendelea, hususani yale ya Afrika kupitia utoaji wake wa mikopo iliyozidisha mzigo wa madeni kwa nchi hizo.