1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michuano ya kombe la EURO kwa wanawake kuanza England

Admin.WagnerD5 Julai 2022

England ndio mwenyeji wa mashindano ya kombe la EURO 2021 kwa wanawake yanayoanza Jumatano (06.07.2022). Mechi ya ufunguzi itakuwa ni kati ya wenyeji England, The Lioness, na Austria.

https://p.dw.com/p/4DhIk
UEFA Frauen EM 2022
Picha: Matt Wilkinson/Stella Pictures/IMAGO

Mechi ya ufunguzi inachezwa Jumatano (06.07.2021) kati ya England The Lioness na Austria katika uwanja wa Old Trafford na fainali itachezwa uwanjani Wembley Julai 31. Mechi ya ufunguzi itavunja rekodi ya mashabiki 41,000 kujitokeza uwanjani kutazama mechi, kwa zaidi ya mashabiki 30,000, katika mashindano ya EURO, huku mashabiki karibu 90,000 wakitarajiwa kuwa uwanjani kutazama mtanange wa fainali huko Wembley.

Idadi kubwa ya mashabiki wanatarajiwa kutazama mechi na kufuatilia mashindano haya, kwa matumaini kwamba mashindano haya yataimarisha soka la wanawake kulifikisha katika ngazi nyingine tofauti ya juu. Nyakati zimebadilika na zinaendelea kubadilika. Wachezaji wana hamasa kubwa kwamba mashabiki watajitokeza kwa wingi kutazama soka la wanawake, hata watoto wadogo.

Baada ya kugubikwa kwa muda mrefu, hatimaye wachezaji wa soka wanawake wa Ulaya wana fursa kwa mara nyingine tena kung'ara na kutamba katika kipindi hiki chote cha michuano ya kombe la EURO.

Takriban tiketi milioni moja zimeshauzwa kwa mashabiki katika nchi 100 kote ulimwenguni, huku tiketi zote za mechi ya leo ya ufunguzi zikiwa zimenunuliwa zote.

Wenyeji England wamepigwa kumbo na kutolewa nje ya mashindano ya EURO katika nafasi ya nusu fainali. Safari hii wanakabiliwa na kibaua kigumu kuhakikisha wanavuka kiunzi na kutimiza matarajio ya mashabiki wao washinde taji la kwanza la mashindano makubwa katika udongo wa nyumbani.

UEFA Frauen EM 2022
Picha: Matt Wilkinson/Stella Pictures/IMAGO

The Lioness wana bahati ya kuwa na kocha Mholanzi Sarina Wiegman, ambaye aliiongoza Uholanzi kushinda kombe la EURO mwaka 2017. Uzoefu huu unatarajiwa huenda pengine ukawasaidia England kupata matokeo mazuri. Kocha Wiegman amesema kikosi chake kiko katika fomu nzuri sana. Hajashindwa katika mechi 14 kama kocha wa England tangu alipochukua mikoba Septemba mwaka uliopita.

Norway ni kitisho kwa wenyeji England

Norway inatarajiwa kuwa tishio kubwa kwa England katika kundi A, huku mshindi wa zamani wa tuzo ya mchezaji bora wa soka duniani upande wa wanawake, Ada Hagerberg, akiwa amerejea kikosini baada ya kujipeleka mwenyewe uhamishoni na kupumzika kutokana na soka la kimataifa kwa miaka mitano.

Uhispania ndio wanaopigiwa upatu kushinda kombe mwaka huu kwa kuwa wanajivunia wachezaji chipukizi wenye vipaji ambao wameigeuza Barcelona kuwa nguvu kubwa katika soka la vilabu vya wanawake. Lakini Uhispania wako katika kundi la kifo pamoja na washindi mara nane Ujerumani na Denmark ambao walifanikiwa kufika fainali mwaka 2017.

Pambano kati ya Uholanzi na Sweden katika kundi C pia litaangaziwa sana katika mechi za makundi. Nyota wa Uholanzi na Arsenal Viviane Miedema amesema msimu huu wa kiangazi ni mojawapo ya fursa kubwa kabisa kuliweka soka la wanawake katika ramani ya soka la dunia.

Ufaransa, Italia, Ubelgiji na Iceland zinacheza katika kundi D, ambalo linaonekana kuwa na wizani sawa. Hata hivyo hatua ya kupanga mechi za kundi hilo kuchezwa katika uwanja wa chuo cha mpira cha klabu ya Manchester City wenye nafasi 4,400 za mashabiki kuingia kutazama mechi, ni jambo ambalo limekosolewa vikali na kiungo wa Iceland, Sara Bjork Gunnarsdottir, ambaye amesema ni kukosa heshima.

(afpe)