1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olimpiki Paris 2024: China yaongoza kwa medali za dhahabu

2 Agosti 2024

Katika Michezo inayoendelea ya Olimpiki huko nchini Ufaransa, China inaendelea kushikilia uongozi wa jedwali la medali.

https://p.dw.com/p/4j1O2
Wanamichezo walioiwakilisha China katika Michezo hiyo ya Olimpiki ya Paris 2024
Wanamichezo walioiwakilisha China katika Michezo hiyo ya Olimpiki ya Paris 2024Picha: Steph Chambers/Getty Images

China bado iko kileleni na jumla ya medali 11 za dhahabu, 7 za fedha na 5 za shaba. Marekani iko katika nafasi ya pili na  medali 9 za dhahabu , 14 za fedha na 13 za shaba. Ufaransa inashikilia nafasi ya tatu ikifuatiwa na Australia na wote wakiwa wamejikusanyia kila mmoja medali 8 za dhahabu. Ujerumani bado iko katika nafasi ya kumi na medali 2 tu za dhahabu.

Katika mchezo wa kuogelea, raia wawili wa Australia Mollie O'Callaghan na Ariarne Titmus walishinda katika mchuano wa kuogelea mita 200 mara nne katika Michezo ya Olimpiki ya Paris hapo jana na kuwabwaga waogeleaji kutoka Marekani na China.

Mnara wa Eiffel ukiwa na nemba za Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024
Mnara wa Eiffel ukiwa na nemba za Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024Picha: David Davies/empics/picture alliance

Mbali na kupata ushindi huo, wawili hao walishikilia pia rekodi ya dunia kwa kuogelea kwa dakika 7 sekunde 38 dhidi ya Wamarekani waliokamilisha zoezi hilo kwa dakika 7:40 huku Wachina wakishikilia nafasi ya tatu kwa kumaliza baada ya dakika 7:42.

Soma pia: Michuano ya Michezo ya Olimpiki Paris 2024 yaendelea

Mfaransa Léon Marchand mwenye umri wa miaka 22, ambaye tayari ni bingwa mara tatu wa michezo ya Olimpiki, atashindana hii leo katika fainali ya kuogelea mita 200, ikiwa ni siku moja baada ya kujipatia ushindi mara mbili wa kuogelea mita 200.

Hata hivyo Léon Marchand anakabiliwa na wapinzani wakubwa  katika fainali hiyo ya kuogelea itakayoshuhudiwa leo usiku. Kwanza ni Carson Foster wa Marekani ambaye amekuwa akifanya vizuri pia. Yupo pia Muingereza Duncan Scott  na Mchina Wang Shun.

Mechi ya robo fainali ya mchuano wa Tennis

Raia wa Serbia Novak Djokovic ameibuka mshindi huko Roland-Garros kwa kumchapa Mgiriki Stefanos Tsitsipas 6-3, 7-6  na 7/3. Hata hivyo Djokovic ameelezea wasiwasi wake kutokana na maumivu kwenye goti lake la kulia, alilofanyiwa upasuaji mwezi Juni, baada ya kuhisi "maumivu makali" wakati wa ushindi wake huo.

Mcheza Tennis maarufu na raia wa Serbia Novak Djokovic
Mcheza Tennis maarufu na raia wa Serbia Novak DjokovicPicha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Djokovic atapambana hii leo na Muitaliano Lorenzo Musetti anayeshikilia nafasi ya 16 duniani na ambaye hivi majuzi alimshinda huko Wimbledon kabla ya kuburuzwa na Carlos Alcaraz katika mechi ya fainali. Djokovic mchezaji maarufu wa Tenis anayeshikilia rekodi ya kuwa na mataji mengi ya Grand Slam yanayofikia 24, hajawahi kushinda medali ya dhahabu ya Olimpiki, jambo ambalo amelifanya kuwa lengo lake kuu.

Soma pia: Kerber afuzu kwa robo fainali ya tenis katika Olimpiki

Daima katika Tennis, mchezaji wa Scotland Andy Murray, ambaye alikuwa ametangaza kwamba angestaafu mwishoni mwa mashindano haya ya Olimpiki, alicharazwa yeye na mwenzake Dan Evans katika mchuano wa robo-fainali huko Roland Garros baada ya Wamarekani Taylor Fritz na Tommy Paul kuibuka na ushindi.

Na kwa uchache katika mpira wa kikapu upande wa wanawake, hapo jana, timu ya Ubelgiji walipambana vilivyo na Marekani lakini walipoteza mechi hiyo kwa kufungwa 87 dhidi ya 74 kwenye Uwanja Pierre-Mauroy huko Villeneuve-d'Ascq.

(Vyanzo: Mashirika)