1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo wa marubani nchini Kenya waingia siku ya tatu

Shisia Wasilwa
7 Novemba 2022

Mgomo wa marubani nchini Kenya unaingia siku ya tatu, licha ya waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen kuonya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

https://p.dw.com/p/4J8mG
Kenya Airways kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya marubani wanaogoma
Kenya Airways kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya marubani wanaogomaPicha: picture-alliance/dpa

Hali ya suitafahamu inazingira uwanja wa kimataifa wa Jommo Kenyatta tangu Jumamosi saa kumi na mbili asubuhi, pindi tu marubani walipoamua kugoma wakitaka nyongeza ya mishahara na marupurupu…Makumi kwa maelfu ya wasafiri wakiduwaa wasijue la kufanya ila kulalamika na kujuta…zaidi ya tani 300 za bidhaa ambazo zilistahili kusafirishwa tayari zimeharibika. Kufikia sasa wasafiri 12000 waliokuwa wamelipa nauli wameathirika Kama wanavyoelezea wasafiri hawa.

"Leo tulistahili kuelekea Mauritious, lakini yaeekea kuwa safari yetu imefutiliwa mbali, ni sawa tu.”,alisema kwa huzuni Jane

"Mimi ni Afisa Mkuu mtendaji wa kampuni moja iliyoko Accra Ghana, Halmashauri ya wakurugenzi ingenipiga kalamu, iwapo hali ingekuwa hivi kwa kampuni yangu,  Afisa mkuu wa Kenya Airways anastahili kujiuzulu pamoja na waziri wa uchukuzi.”,alisema habiria mwingine.

Haya yanajiri huku taarifa zikisema kuwa shirika la ndege la Kenya halijalipa mkopo wa shilingi bilioni 102 za Kenya kutoka Marekani. Wasafiri kadhaa wamelipiwa kusafiri kwa ndege za mashirika mengine huku wengine wakilipiwa hoteli kabla ya suluhisho kutafutwa.

"Baadhi ya matakwa yao, yanahitaji fedha''

Shirika ndege la Kenya linasema lilighairi safari 56 za ndege mwishoni mwa juma
Shirika ndege la Kenya linasema lilighairi safari 56 za ndege mwishoni mwa jumaPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika hilo Allan Kilavuka amewaonya marubani hao wanaogoma. Kilavuka ameongeza kusema kuwa shirika hilo lilikuwa limepiga hatua tangu janga la Covid, lakini sasa mgomo huo unaathiri juhudi zilizokuwa zimefanywa. Amesisitiza kuwa mgomo huo ni haramu na unajiri wakati mbaya.

"Baadhi ya matakwa yao, yanahitaji fedha. Wanataka tuyatimize mara moja, tunasema wakitaka tuyatimize matakwa yao, kwanza warudi kazini.”

Chama cha marubani cha shirika hilo hakijaelezea mgomo huo utakamilika lini. Hata hivyo kimeshikilia kuwa marubani wake watarejea kazini pindi tu mfuko wa malipo yao utakaporejeshwa pamoja na nyongeza ya mishahara.   Shirika hilo limesema kuwa linakadiria hasara ya shilingi milioni 300 kwa siku, kwa juma moja fedha hizo zitafikia shilingi bilioni 2.1. Hata hivyo safari za Adis Ababa, Entebbe na Mombasa pamoja na Lusaka, hazijafutiliwa mbali. Asilimia 80 ya Shirika la ndege la Kenya inamilikiwa na serikali huku asilimia 20 ikimilikiwa na shirika la ndege la Air France-KLM.