1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Umoja wa Ulaya na Belarus unazidi kuongezeka

9 Novemba 2021

Mgogoro uliopo katika mpaka wa Belarus na Poland, hauonyeshi dadlili yoyote ya kupungua huku pande zote mbili zikitupiana lawama, wakati wahamiaji wengi waliokosa makaazi wakikwama katika eneo lenye baridi kali.

https://p.dw.com/p/42mUV
Migranten an der Grenze Belarus - Polen
Picha: Leonid Scheglov/BelTA/REUTERS

Kwa sasa wahamiaji wengi wanakumbwa na baridi kali katika eneo la mpakani, kati ya Poland na Belarus, wakati Poland  ikiushutumu utawala wa Belarus kwamba inawatumia wahamiaji kutishia usalama wa nchi za Umoja wa Ulaya.

Kwa miezi sasa Umoja wa Ulaya umekuwa ukiituhumu serikali ya mjini Minsk kwamba inawaelekeza wahamiaji wanaojaribu kuingia kwenye nchi za Umoja huo katika nchi za  Poland,Latvia na Lithuania na hata wale waliokuwa wakiomba hifadhi kwenye nchi nyingine za maeneo ya migogoro,hatua hiyo ikiwa kama ya ulipizaji kisasi vikwazo ilivyowekewa na nchi za Magharibi kutokana na ukandamizaji wake wa kisiasa nchini mwake.

Belarus imekanusha madai hayo na kuishutumu Poland kwa kukiuka haki za binaadamu kwa kukataa kuwapokea wahamiaji. Hali hiyo ya wasiwasi imezua hofu ya kutokea mvutano zaidi katika eneo la mpakani ambako kumeonekana  maaskari wa pande zote mbili waliojihami.

Hali imekuwa tete baada ya wahamiaji kukimbilia katika mpaka wa Poland

Belarus Migranten im Grenzgebiet zu Polen
Wahamiaji katika mpaka wa PolandPicha: Leonid Shcheglov/BelTA/AP/dpa/picture alliance

Mgogoro ulitanuka zaidi hapo jana wakati wahamiaji walipoelekea mpakani wakitaka kuingia Poland walikozuwiwa na mamlaka ya taifa hilo. Belarus na Poland zimesema kati ya wahamiaji 3,000 hadi 4,000 sasa wamepelekwa katika kambi ya muda karibu na kijiji cha Kuznica nchini poland. Waandishi habari wamenyimwa ruhusa  ya kuingia huko lakini vidio zinazosambazwa na utawala wa pande hizo mbili hasimu, zimewaonyesha wahamiaji wakisimama katika ukuta wa nyaya uliopo mpakani, wakiota moto ili kupunguza baridi kali iliyoko na wengine wengi wakiwa ndani ya makambi.

Poland imeendelea kusisitiza kuwa Belarus inawatumia wahamiaji kama ngao na kusema kamwe haitofungua mipaka yake.  Waziri Mkuu wa taifa hilo Mateusz Morawiecki amesema Uthabiti na usalama wa Ulaya uko hatarini maana shambulizi linalofanywa na utawala wa Lukashenko limenuiwa kumdhuru kila mtu. Ameongeza kuwa hawatotishwa na wataendelea kuitetea amani ya Ulaya pamoja na washirika wake Jumuiya ya kujihami NATO na Umoja wa Ulaya EU.

Kauli kali ya NATO kwa Belarus

Hapo jana Marekani na NATO zimeishutumu Belarus, kupanga wimbi kubwa la wahamiaji na kuitaka iache mara moja kufnya hivyo. Umoja wa Ulaya nao umeitaka Belarus kuwekewa vikwazo zaidi, baada ya awali Lukashenko kuwekewa vikwazo kufuatia kamatakamata dhidi ya wanachama wa upinzani baada ya uchaguzi uliokuwa na utata mwaka uliopita.

Ufaransa nayo pia imepaza sauti yake juu ya mgogoro huu. Kupitia Wizara yake ya mambo ya kigeni, imesema Belarus inajaribu kulisambaratisha bara la Ulaya

Huku hayo yakiarifiwa Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema matukio yanayofanywa na majeshi ya magharibi ndio yanayochangia wimbi kubwa la wakimbizi. Amesema kutatua tatizo hilo kunategemea pakubwa na wale walilolianzisha. Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa linalowashugulikia wakimbizi limesema linaangalia hali kwa karibu na lina wasiwasi juu ya hatma ya wahamiaji hao.

 

Chanzo: DAA/AFP/RTR