1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa kugawana wizara nchini Zimbabwe

Kalyango Siraj17 Oktoba 2008

Mugabe kachukua wizara 'muhimu',Tsvangirai asema haiwezekani

https://p.dw.com/p/FcDz
Tsvangirai-kushoto,Mugabe-kuliaPicha: AP

Mgogoro wa kugawana madaraka kati ya vyama viwili vikuu nchini Zimbabwe baado unaendelea licha ya kufanyika kwa mazungumzo ya kuutanzua.Kila upande unaulaumu mwingine kwa kusababisha mkwamo wa kundwa kwa serikali ya mseto kufuatiwa kutia saini makubaliano ya kugawana madaraka mwezi uliopita.

Awamu nyingine ya mazunguzo ya kugawana madaraka imefanyika mjini Harare ambayo ni siku ya nne mfulululizo.Mazungumzo ni kati ya rais Robert Mugabe,Morgen Tsvangirai na kiongozi mwingine Arthur Mutambara.

Rais Mugabe alipowasili sehemu ya mkutano amewambia waandishi habari kuwa leo Ijumaa ni siku ya maafikiano.Lakini mpinzani wake Tsvangirai,alionekana muangalifu kukubali kuwa kutafikiwa muafaka,ila alisema tu kuwa wote wanamatumaini.

Awamu hii inakuja kukiwa na shinikizo la kimataifa kwa pande husika kumaliza mkwamo wa kugawana wizara nyeti.Shinikizo linakuja huku kila upande ukiulaumu mwingine kwa kuzorotesha mazungumzo yanaongozwa na rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki.

Chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change MDC cha Morgen Tsvangirai kimesema leo kuwa Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Afrika vitahitajika kuingilia kati ikiwa mazungumzo ya kugawana madaraka kuhusiana wizara zinazoitwa nyeti hautafumbuliwa.

Na wanachama wa chama cha rais Mugabe cha ZANU PF wanakilaumu chama cha MDC kwa kile walichoita 'imani potovu' katika mazungumzo yanayoendelea na kutaka kuingiza Umoja wa Mataifa katika masuala hayo.Gazeti la serikali ' The Herald ' limewanukuu maafisa wa ZANU PF kusema kuwa MDC inadumaza mazungumzo hayo kumfanya Mbeki ashindwe ili Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa viingilie kati. Aidha rubaa za gazeti hilo zimesema kuwa Tsvangirai anapata maelekezo kutoka kwa Marekani na Uingereza.

Pia Tsvangirai analaumiwa kwa kutaka kuzusha upya mjadala wa kugawana wizara ambao tayari ulitanzuliwa.

Tangu kutia saini makubaliano ya kugawana madaraka septemba 15, kumekuwa na mkwamo kuhusina nani achukue wizara ya mambo ya ndani,ambayo inasimamia jeshi la polisi.Wiki iliopita rais Mugabe alikigawia chama chake cha ZANU-PF wizara muhimu mkiwemo wizara za fedha, ulinzi na mambo ya ndani.Ikiwa wizara za mambo ya ndani na ulinzi zitakuwa mikononi mwake hiyo inampa udhibiti wa vikosi vyote vya usalama vya nchi hiyo.

Lakini Tsvangirai anasisitiza kuwa udhibiti wa vikosi vya usalama ni lazima ugawanywe sawa.Ingawa alikubali kuwa wizara ya Ulinzi ichukuliwe na ZANU-PF yeye angetaka chama chake kisimamie wizara ya mambo ya ndani.Na wiki iliopita alionya kujiondoa katika mazungumzo hayo ikiwa chama chake hakitapewa wizara ya mambo ya ndani.

Na hayo yakiendelea, Marekani imeonya kuwa huenda ikaiwekea vikwazo zaidi serikali ya Mugabe ikiwa mpango wa kugawana madaraka utashindwa.

Onyo hilo limetolewa na mjumbe maalum wa Marekani barani Afrika Jendayi Frazer akiwa katika ziara maalum nchini Japan.

Onyo kama hilo lilitolewa na mawaziri wa kigeni wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wao wa Luxembourg mapema wiki hii.Mawaziri hao walionya vikwazo zaidi kwa Zimbabwe ikiwa Mugabe hataheshimu makubaliano hayo.