1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Warundi wapinga mfumo wa kuendesha nchi kikabila

2 Agosti 2023

Mkutano ulioandaliwa kwa ushirikiano wa Baraza la Seneti nchini Burundi kuzungumzia endapo uwakilishi wa makabila katika taasisi rasmi za nchi hiyo ya kati mashariki mwa Afrika uendelee ama ufutiliwe mbali umemalizika.

https://p.dw.com/p/4UgEm
Uganda EAC Wahlbeobachtermission
Picha: Lubega Emmanuel/DW

Mkutano huo ulihitimishwa kwa wengi miongoni mwa washiriki kuunga mkono utaratibu huo uondolewe. Msimamo unaopigwa vikali na wanasiasa wa upinzani.

Miongoni mwa waliojitokeza wazi kupinga uamuzi wa kuufuta utaratibu huo, alikuwa ni makamu wa zamani wa rais, Gaston Sindimwo, amesema mkakati huo wa usawa kikabila katika taasisi rasmi za nchi uliazimiwa katika Mkataba wa Amani wa Arusha ili kuhakikisha makabila yote yawakilishwa katika uendeshaji wa nchi na kwamba Burundi haijawa tayari kuachana na mfumo huo, alioutaja kama msingi wa amani inayoshuhudiwa sasa:

Mfumo wa makabilia katika kuendesha nchi umepitwa na wakati.

Malawi | Dzaleka Flüchtlingslager
Baadhi ya wakimbizi wa Burundi wakiwa katika kambi ya wakimbizi ya Dzaleka MalawiPicha: Amos Gumullira/AFP/Getty Images

Awali, kikao hicho kilichoandaliwa na Baraza la Seneti na kuwashirikisha maafisa wa makabila na asasi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mawaziri wa serikali, asasi za kiraia, rais wa zamani na baadhi ya raia wa kawaida kilijumuisha maoni mengi ya wajumbe walioashiria kuwa kushiriki katika taasisi za nchi kwa misingi ya kikabila ni mfumo unaoelekea kupitwa na wakati:

Mshiriki mmoja katika mkutano huo alisikika akisema "Naunga mkono mia kwa mia kuwa mfumo huo uondolewe, kwani itafikia nyakati maswala ya kabila yatakuwa hayapo tena nchini. Lakini kinachohitajika ni maandalizi ya kutosha ili tufikie hapo.

Kuna shughuli muhimu zilizotakiwa kwanza kukamilishwa, kwenye tume ya ukweli na maridhiano, shughuli za tume ya kutatuwa mizozo ya ardhi na mali nyingine, pamoja na kuandikwa historia rasmi ya Burundi."

Rais wa zamani wa Burundi Domitien Ndayizeye anasema vita dhidi ya umasikini ni muhimu zaidi.

Domitien Ndayizeye, rais wa zamani ambaye pia ni mmoja ya walioshiriki majadiliano yaliyofikia usainiwaji wa Mkataba wa Amani wa Arusha, ameiambia hadhara iliyoshiriki mkutano huo kuwa, endapo vita dhidi ya umasikini vitafanikiwa, hakutakuwa na raia  atakayezusha swala la ukabila:

"Kamwe sitoweza kutoka kwangu kana kwamba nakwenda kulipigania kabila, wakati sote tutakuwa tunapata lishe ya kutosha. Na wala hakuna atakayeleta swala la ubaguzi wakati na yeye atakuwa anapata chakula cha kutosha. Lakini tukisalia katika umasikini, itakuwa vigumu kuondoa katika hisia za watu swala la ubaguzi."

Soma zaidi:Changamoto za kuwahudumia wakimbizi wa Kongo

Mfumo huo wa uwakilishi wa kikabilia uliwekwa na Mkataba wa Amani wa Arusha uliofikiwa mwaka 2000 nchini Tanzania na kuingizwa katika katiba ya nchi ukiagiza Wahutu kuwakilishwa katika taasisi kwa asilimia 60, Watutsi kwa asilimia 40 na wanawake kwa asilimia 30. Lengo likiwa ni kukomesha mtengano wa kikabila.

Maazimio ya mkutano huu wa tathmini uliotishwa na Baraza la Seneti yatakabidhiwa serikali kwa utekelezaji.

DW: Burundi