1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfalme Philippe aendelea na ziara yake Congo

Sylvia Mwehozi
8 Juni 2022

Mfalme Philippe wa Ubelgiji ameendelea na ziara yake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo siku ya Jumatano amerejesha kinyago cha utamaduni katika koloni lake la zamani huku akitarajiwa kulihutubia bunge.

https://p.dw.com/p/4CQZD
Belgisches Königspaar zu Besuch in der Republik Kongo
Picha: Benoit Doppagne/BELGA/IMAGO

Mfalme Philippe aliwasili nchini Congo akiwa na mkewe Malkia Mathilde na waziri mkuu Alexander De Croo, kwa ziara ya wiki moja. Katika mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari na waziri mkuu De Croo, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi amesema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano na Ubelgiji sambamba na kuvutia zaidi wawekezaji, kuboresha huduma za afya na elimu nchini Congo. Eddy maziba ni mwanahistoria na mchambuzi wa kisiasa ana mtizamo huu kuhusu ziara hiyo. "Kwangu mimi, ziara ya mfalme wa Ubelgiji ina umuhimu mkubwa kwa sababu katika nyakati hizi, Afrika inaanza kurejesha hazina yake iliyoporwa wakati wa ukoloni, hivyo ziara ya mfalme wa Ubelgiji ni ya manufaa"

Mnamo mwaka 2020, Mfalme Philippe alikuwa afisa wa kwanza wa Ubelgiji kuelezea majuto ya "mateso na fedheha" dhidi ya Congo. Hata hivyo hakuomba radhi na baadhi ya raia wa Congo wametaka kiongozi huyo kufanya hivyo wakati wa ziara yake ya kwanza tangu achukue madaraka mwaka 2013.

DR Kongo | Besuch Philippe, König der Belgier | Schaulustige
Raia wa Congo waliojitokeza kumlaki Mfalme PhilippePicha: Nicolas Maeterlinck/Belga Photo/AFP/Getty Images

Hii leo Mfalme Philippe amerejesha kinyago cha watu wa jamii ya Suku katika makumbusho ya taifa ya Congo. Kinyago hicho kimekuwa kikishikiliwa kwa miongo kadhaa katika makumbusho ya kifalme ya Ubelgiji.

"Kazi hii nzuri ya sanaa ni mkopo usio na ukomo kutoka makumbusho ya kifalme ya Tervuren ya Afrika ya Kati kwa jumba la makumbusho ya kitaifa ya Kinshasa ambayo inaweza kuijenga upya. Inaashiria mwanzo wa uimarishaji wa ushirikiano wa kitamaduni kati ya Ubelgiji na Congo," alisema Mfalme Philippe.

Mbali na hilo pia, Mfalme Philippe amemtunuku nishani ya heshima ya juu manusura pekee aliyeshirika vita vya pili vya duniani Koplo Albert Kunyuku, ambaye sasa ana umri wa miaka 100. Kunyuku alipigana huko Burma wakati wa vita vya pili kwa niaba ya Ubelgiji.

Baadhi wanakadiria kuwa mauaji, njaa na magonjwa viliuawa Wakongo takribani milioni 10 katika kipindi cha miaka 23 tu ya utawala wa Ubelgiji kutoka mwaka 1885 hadi 1960, wakati Mfalme Leopold II alipoitawala Congo kama milki yake binafsi.

Baada ya Leopold kudai umiliki wake kumalizika mwaka 1908, aliikabidhi kwa serikali ya Ubelgiji, ambayo iliendelea kutawala hadi ilipopata uhuru mwaka 1960.