1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Messi, Neymar, Mbappe hawakufua dafu

4 Oktoba 2021

Licha ya kuwa na safu ya mashambulizi inayodaiwa kuwa ya kutisha zaidi duniani kwa sasa, inayowajumuisha Lionel Messi, Neymar na Kylian Mbappe, Paris Saint Germain walinyamazishwa 2-0 na Stadde Rennes

https://p.dw.com/p/41FIe
Leo Messi Paris Saint Germain v Olympique Lyonnais
Picha: Jose Breton/NurPhoto/imago images

Licha ya kuwa na safu ya mashambulizi inayodaiwa kuwa ya kutisha zaidi duniani kwa sasa, inayowajumuisha Lionel Messi, Neymar na Kylian Mbappe, Paris Saint Germain walinyamazishwa 2-0 na Stadde Rennes katika mechi ya Ligue 1 na washambuliaji watatu hao hawakusajili shuti hata moja lililolenga lango katika kipindi chote cha dakika tisini.

Licha ya kumsajili Messi, PSG waliwasajili Gianluigi Donnaruma, Achraf Hakimi, Georgino Wijnaldum na Sergio Ramos jambo lililowapa matumaini mashabiki wao kwamba mambo yatakuwa rahisi na watashinda kila mechi, ila sivyo mambo yalivyokuwa mwishoni mwa wiki.

Huko England nako umahiri wa Mohammed Salah haukutosha kuwapa Liverpool pointi zote tatu walipokuwa wanachuana na Manchester City uwanjani Anfield.

Mohamed Salah I Liverpool
Nyota wa Liverpool Mohamed SalahPicha: picture-alliance/AP/S. Botterill

Raia huyo wa Misri ambaye alimuandalia Sadio Mane goli la kwanza alipachika wavuni bao la pili baada ya kuwapiga vyenga na kuwalambisha nyasi mabeki wa Manchester City, goli hilo likitajwa kama mojawapo ya magoli bora zaidi hadi msimu ulipofikia sasa.

Lakini Manchester City walifungiwa mabao yao na Phil Foden na Kevin De Bruyne na kuhakikisha kwamba hawaondoki mikono mitupu hapo Anfield.