Merkel akutana na viongozi wa Poland
8 Februari 2017Merkel alikutana na mwanasiasa mwenye nguvu zaidi nchini Poland Jaroslaw Kaczynski, lakini hakukuwa na ufafanuzi juu ya nini walichokizungumza, ingawa Kaczynski alisema mkutano wao ulikuwa chanya. Baada ya dakika 60 za mazungumzo na Merkel, mwenyekiti wa chama tawala cha Sheria na Haki (PiS) Jaroslaw Kaczynski alisema kulikuwepo na mazingira mazuri.
Kaczynski, mwanasiasa asiye na imani kabisa na Ujerumani, aliwahi kusema kwamba lengo la Merkel ni kuifanya Poland kuwa chini ya Ujerumani. Merkel aliitolea mwito serikali ya mrengo mkali wa kulia ya Poland kulinda haki za upinzani wa kisiasa na pia za mfumo wa kisheria, vyama vya wafanyakazi na vyombo vya habari, wakati ambapo Umoja wa Ulaya unachunguza uwezekano wa ukiukaji wa kanuni za utawala wa sheria nchini Poland.
"Tunajua umuhimu wa jamii za watu wenye mawazo mbalimbali, uhumimu wa mahakama na sekta ya habari vilivyo huru, kwa sababu hivyo vyote vilikuwa vinakosekana zamani. Na ndiyo sababu nimefurahi kusikia kwamba Poland pia itajibu maswali ya halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya," alisema Merkel.
Vikwazo vya Urusi kuendelea
Katika mazungumzo tofauti na waziri mkuu wa Poland Beata Szydlo, Merkel aligusia mgogoro unaoendelea nchini Ukraine. Kansela huyo baadae akawaambia waandishi habari kwamba vikwazo dhidi ya Urusi kuhusiana na mgogoro huo haviwezi kuondolewa, akiongeza kuwa hali ndani ya eneo la mashariki mwa Ukraine haikubaliki.
Matamshi ya Merkel yalikuja saa chache tu baada ya mazungumzo alioyafanya kwa njia ya simu na rais wa Urusi Vladmir Putin ambamo alimsihi kutumia ushawishi wake mashariki mwa Ukraine kukomesha vurugu zilizodumu kwa karibu miaka mitatu sasa. Viongozi hao wawili hata hivyo walikubaliana juu ya haja ya juhudi mpya za usitishaji mapigano.
Licha ya kukubaliana linapokuja suala la Urusi, mradi unaobishaniwa wa ujenzi wa bomba na mafuta la Nord Stream mbili unaendelea kusababisha ugomvi kati ya Poland na Ujerumani. Akirudia msimamo wa nchi yake siku ya Jumanne, waziri mkuu Szydlo alisema ujenzi wa bomba hilo haukubaliki kwa Poland. Chini ya makubaliano ya mradi huo kampuni ya nishati ya Urusi ya Gazprom, itafikisha bomba hadi nchini Ujerumani, likizipita Poland, mataifa ya Baltic pamoja na Ukraine.
Mageuzi ndani ya Umoja wa Ulaya, mustakabali wa NATO
Viongozi hao pia walizungumzia mageuzi ndani ya Umoja wa Ulaya. Wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi habari, Szydlo alisema Poland imedhamiria kuendeleza mahusiano yake na Ujerumani, na kuongeza kuwa anaanimini uhusiano kati ya Ujerumani na poland ni muhimu kwa mafanikio ya mradi wa Umoja wa Ulaya.
Merkel pia alizungumzia matamshi yaliotolewa na rais wa Marekani Donald Trump na waziri wake wa ulinzi kuhusu jumuiya ya kujihami NATO - waliposema kwamba Marekani inaiunga mkono kwa dhati jumuiya hiyo, na kusema matamshi ni muhimu, na kwamba watakuwa na fursa ndani ya NATO kuzungumzia mustakabali na changamoto.
Mawaziri wa ulinzi wa jumuiya ya NATO wanatarajiwa kukutana na waziri mpya wa ulinzi wa Marekani kwa mara ya kwanza wiki ijayo, na tena katika mkutano wa kimataifa wa usalama mjini Munich wiki moja baadae.
Mwandishi:Gerhard Gnauck/Iddi Ssessanga
Mhariri: Bruce Amani