1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Rutte wajadili mageuzi ya Ulaya

Josephat Charo
10 Julai 2020

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameutolea mwito Umoja wa Ulaya kufanya mageuzi ya kijasiri mwanzoni mwa mkutano wake na Waziri Mkuu wa Uholanzi, Mark Rutte Alhamis (09.07.2020).

https://p.dw.com/p/3f8xK
Berlin Mark Rutte bei Merkel
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. von Jutrczenka

Msaada ambao hautahusishwa na mageuzi na kujielekeza katika siku zijazo mwishowe hautasaidia chochote, alisema Merkel, wakati wakijadili mgawanyiko uliopo kwa nchi za Ulaya baada ya kutokea mlipuko wa virusi vya corona.

Kansela Merkel aliongeza kusema kuwa baada ya mtikisiko kutokea kufuatia mlipuko wa janga la virusi vya Corona, itakuwa wazi ni nani anayeweza kuhakikisha ustawi wa watu, kitu ambacho kitawezekana tu kukiwepo na uchumi imara na wenye ushindani.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uholanzi, Rutte, amekiri bayana kuwa janga la virusi vya Corona limesababisha madhara makubwa na kuongeza kuwa kwa sasa ni muhimu sana kwamba tunashughulikia tatizo hili ambalo nchi za Ulaya kwa pamoja zinakabiliana nazo.

Ujerumani na Uholanzi zinaweza kusonga mbele kama nchi zote za Jumuiya ya Ulaya zitafanya vizuri, alisema Rutte akibainisha kuwa mfumo wote wa uchumi umeunganishwa kwa ukaribu sana.

Mkutano huo ulifanyika kuelekea mkutano mkuu wa kilele wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika mnamo Julai 17 hadi 18 mwaka huu ambapo watu wengi wanatarajia ishara ya makubiliano juu ya azma ya Halmashauri ya Ulaya ya kufufua mfuko wenye thamani ya euro bilioni 750 sawa na dola za Kimarekani bilioni 851.

Hii inajumuisha euro bilioni 500 katika misaada na euro bilioni 250 kwa mikopo kusaidia urejeshaji uchumi wa nchi za Umoja wa Ulaya. Mataifa ya Uholanzi pamoja nna Denmark, Sweden na Austria yangependelea mikopo badala ya misaada na pesa kuunganishwa na mageuzi ya kiuchumi.

Rutte asisitiza umuhimu wa nguvu za kiuchumi

Alhamis iliyopita, Rutte alisisitiza umuhimu wa mfuko wa uokoaji wa Umoja wa Ulaya lakini akasema hii inapaswa kufanywa pamoja na mageuzi ili nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya pia ziwe na nguvu.

Akiangazia zaidi mfumo wa kifedha wa kati wa Umoja wa Ulaya, Rutte alisema jumuiya hiyo inapaswa kuwa na nguvu na kuongeza kuwa hawataki mchango wa jumla kuongezeka sasa kama matokeo ya Brexit na virusi vya Corona.

Rutte alisema anataka Ulaya ya kijani na ya kidijitali, lakini pia jumuiya hiyo ambayo inaunga mkono kabisa maadili yake ya kikatiba na sheria ambazo zilikuwa zikiheshimika kila mahali.

Berlin Mark Rutte bei Merkel
Picha: picture-alliance/ANP/B. Grösse

Mazungumzo ya viongozi hao ni kwa ajili ya kuzingatia vipaumbele vya Ujerumani wakati wa kugombea kwake Urais wa baraza la Umoja wa Ulaya. "Tunayo mengi ya kujiamini kuhusu wewe,” Rutte alimwambia Merkel, huku akiitakia Ujerumani mafanikio.

"Lengo letu la kawaida ni kufikia makubaliano mapema iwezekanavyo. Natumai kweli kwamba tunaweza kufikia makubaliano wakati wa majira haya ya kiangazi. Bado inahitaji utashi mwingi na maelewano kutoka pande zote," alisema Rutte.

Wakati huo huo, Rutte, anakabiliwa na shinikizo la ndani kutoka kwa wezi wa fedha nyumbani na ameshikilia msimamo muhimu zaidi kuelekea ombi hilo.

"Msaada kutoka Kaskazini inamaanisha mabadiliko kutoka Kusini. Hakuna njia nyingine," mwanasiasa huyo wa mrengo wa kati alisema wiki iliyopita.

Baada ya Merkel, Rutte anapanga kukutana na wakuu wa serikali za Italia, Uhispania na Ureno kujadili mpango wa kuufufua uchumi. Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte anatarajiwa kuwasili nchini Uholanzi kwa mazungumzo Ijumaa, msemaji wa serikali alisema Alhamisi huko mjini The Hague.

Ziara hiyo inatarajiwa kufuatiwa na mazungumzo ya wakati wa chakula cha mchana na waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez mjini The Hague Jumatatu, huku waziri mkuu wa Ureno Antonio Costa akitarajiwa kukutana na Rutte saa chache baadaye.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, alimtembelea Rutte mwishoni mwa mwezi Juni katika ziara kama hii ya ushawishi.

(dpae)