Merkel kukutana na Putin
18 Agosti 2018Putin amewasili nchini Ujerumani baada ya kutembelea shamba la mizabibu nchini Austria kuhudhuria harusi ya waziri wa mambo ya kigeni Karin Kneissl ambaye anaoana na mfanyabiashara Wolfgang Meilinger.
Merkel ameonya jana Ijumaa dhidi ya matarajio makubwa kutoka katika majadiliano yake na Putin katika makao makuu ya serikali ya Meseberg, lakini amesema nchi hizo mbili zinahitaji kuendelea , "kuwa na majadiliano kila mara" kuhusiana na orodha ndefe ya matatizo zinazokabiliana nayo.
"Ni mkutano wa kazi ambao hakuna matokeo maalum yanayotarajiwa," amewaambia waandishi habari. Viongozi hao wawili walikutana mara ya mwisho mjini Sochi mwezi Mei na walishindwa kuondoa tofauti zao.
Lakini Juergen Hardt, msemaji wa sera za mambo ya kigeni katika kundi la vyama vya kihafidhina vinavyoongozwa na kansela Merkel , na Achim Post , mjumbe mwandamizi wa chama cha Social Democrats SPD, chama mshirika katika serikali ya Ujerumani , walikuwa na matumaini.
Hatua zinazochukuliwa
"Tunaweza kwa tahadhari kuwa na matumaini," Hardt aliliambia gazeti la Stuttgarter Zeitung katika mahojiano yaliyochapishwa leo Jumamosi. "rais wa Urusi amejiingiza mwenyewe katika hali ya kufikia mwisho nchini Syria na mashariki mwa Ukraine, na anahitaji washrika wa kimataifa. Kwa hilo anahitaji kuchukua hatua.
Afisa mwandamizi wa serikali ameliambia gazeti : "Kumekuwa na hatua zinazochukuliwa," lakini hakutoa maelezo zaidi.
Post amesema katika taarifa kwamba anatarajia Merkel na Putin kuangalia suluhisho linalowezekana lililo katika misingi ya maslahi ya pamoja. "Katika dunia ambayo inaongezeka hali ya sintofahamu, tunapaswa kuzungumza hususan na washirika ambao ni wenye matatizo kama Urusi," amesema.
Urusi na mataifa ya magharibi zinabaki kutofautiana kuhusiana na hatua ya Urusi kulinyakua jimbo la Crimea kutoka Ukraine mwaka 2014 na kuzuka mzozo kati ya watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo wakipambana na jeshi la Ukraine. Kuhusu Syria , Ujerumani inamtaka Putin kukamilisha makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano nchini humo kwa makubaliano na Marekani. Merkel jana Ijumaa alisema mkutano wa pande nne kuhusu Syria unaoihusisha Ujerumani , Urusi, Uturuki na Ufaransa unawezekana kufanyika.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Jacob Safari Bomani