Merkel asema ni mafanikio madogo katika kupunguza gesi chafu
22 Julai 2021Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amejibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari kwenye kikao chake kinachotarajiwa kuwa cha mwisho cha majira ya joto kabla ya kuondoka madarakani baada ya miaka 16.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amepongeza makubaliano baina ya Marekani na Ujerumani kuhusu mradi tata wa ujenzi wa bomba la gesi wa Nord Stream 2.
Kansela Merkel ameyaita makubaliano hayo ya mradi wa bomba la gesi la Nord Stream Mbili kuwa ni hatua nzuri, licha ya kuweko na tofauti baina ya Marekani na Ujerumani kuhusu mradi huo. Merkel amesema kuwa nchi yake inahitaji mradi huo wa Nord Stream.
''Nafikiri makubaliano na serikali ya Marekani hayajamaliza tofauti, lakini hayajasuluhisha pia tofauti hizo, tofauti bado zimesalia na hali hiyo ilionekana jana. Ni jaribio baina ya serikali ya Marekani na sisi kuweka baadhi ya masharti ''
Hatua hiyo ni katika dhamira ya Marekani na Ujerumani ya kuiwajibisha Urusi kwa ushari wake na shughuli za uovu, kwa kuiwekea vikwazo na kutumia nyenzo nyingine. Makubaliano hayo yamefikiwa siku chache baada ya ziara rasmi ya mwisho ya Angela Merkel mjini Washington kabla ya kuondoka madarakani mwezi Septemba.
Ongezeko la visa vya Covid-19 kwa ''kasi ya kutisha''
Kansela wa Merkel amelezea pia wasiwasi wake kuhusu ripoti za ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona nchini Ujerumani. Merkel amewambiwa wandishi harabi mjini Berlin leo kwamba idadi ya visa inaongezeka kwa kasi ya kutisha.
Merkel amewahimiza wananchi kupata chanjo na kuwataka wale ambao tayari wapepokea chanjo hizo kuwahimizi wengine wafanye hivyo. Amesema mbali na masharti na vizuwizi vya kupamabana na janga la Covid-19, lakini chanjo ndio njia pekee ya kuutokomeza ugonjwa huo.
Athari za mabadilko ya tabianchi
Kufuatia mafuriko yaliyosababisha vifo vya watu 177 kwenye majimbo ya magharibi mwa Ujerumani, Kansela Merkel amesisitizia wito wake wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Merkel amesema kuna mafanikio madogo kuhusu malengo ya kupunguza kwa chini ya nyuzi joto 2 uzalishaji wa gesi chafu.
Akigusia kashfa ya udukuzi ya programu ya Pegasus, inayotengenezwa na kampuni ya Israeli ya teknolojia ya ujasusi wa kimtandao ya NSO, Kansela Merkel ameomba kuweko na masharti kuhusu uuzwaji wa programu za kimtandao. Merkel amesema ni muhimu programu za aina hiyo kutowafikia watu watakaozitumia kwa njia mbaya.