1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel asema Mashambulizi ya kijeshi Syria yanastahili

14 Aprili 2018

 Kansela wa Ujerumani amesema anaunga mkono mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani, Ufaransa na Uingereza nchini Syria akiyataja muhimu na yanayostahili.

https://p.dw.com/p/2w2ig
Merkel empfängt dänischen Ministerpräsidenten Rasmussen
Picha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Wiki hii Kansela huyo wa Ujerumani alisema nchi yake haitashiriki katika hatua ya kijeshi Syria lakini itaunga mkono hatua za kijeshi zitakazochukuliwa na nchi wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Waziri mkuu wa Uingereza Theresa Maya amesema mashambulizi hayo ya Syria ni sawa na halali.

Ufaransa imesema ilifyatua makombora 12 yaliyolenga maeneo kadhaa ya kijeshi Syria na kuongeza watafanya mashambulizi zaidi iwapo silaha za sumu zitatumika tena Syria. Wakati huo huo, waasi wa Syria wamesema mashambulizi hayo ya kijeshi hayana maana kama hayatalenga kumuondoa madarakani Rais Bashar al Assad.

Syrien Damaskus Militärschlag
Mji wa Damascus ulivoonekana wakati wa mashambulizi ya anganiPicha: Imago/Xinhua/A. Safarjalani

Putin alaani, EU yaunga mkono mashambulizi

Rais wa Urusi Vladimir Putin amelaani vikali mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani na washirika wake nchini Syria na kuitisha kikao cha dharura ckha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Putin ameseam mashambulizi hayo ya angani yaliyofanywa mapema leo asubuhi na Marekani, Ufaransa na Uingerezan yanaufanya mzozo wa kibinadamu Syria kuwa hata mbaya zaidi na kuwasababishia raia dhiki na kuharibu mahusiano ya kimataifa.

Rais wa Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk amesema Umoja wa Ulaya unaziunga mkono Marekani, Uingereza na Ufaransa kwa kuchukua hatua za kijeshi Syria dhidi ya utawala wa Syria unaodaiwa kutumia silaha za sumu dhidi ya raia wake. Tusk amesema mashambulizi hayo ya kijeshi yanapaswa kutuma ujumbe bayana kuwa utawala wa Syria na washirika wake Urusi na Iran hawawezi kuendelea na kusababisha majanga bila ya kuchukuliwa hatua.

Marekani, Uingereza na Ufaransa zashambulia Syria

Serikali ya Syria imeyaita mashambulizi ya mataifa ya magharibi kwenye mitambo yake ya kijeshi, kuwa ya kikatili na ya kijinga na kwamba yamekiuka sheria za kimataifa. Marekani, Ufaransa na Uingereza zimefanya mfululizo wa mashambulizi ya angani Jumamosi asubuhi katika maeneo ya karibu na mji mkuu wa Damascus na katikati mwa mji wa Homs.

Zypern Britischer Kampfjet vor Einsatz
Ndege za kivita za UingerezaPicha: picture-alliance/AP Photo/L. Matthews

Operesheni hiyo ya pamoja inakuja wiki moja baada ya shambulizi la kemikali linalodiawa kufanywa kwenye mji unaodhibitiwa na waasi nje kidogo ya Damascus na kuwaua watu 40.

Mataifa ya magharibi yalimtuhumu rais Bashar al Assad kwa shambulizi hilo, lakini Syria na mshirika wake Urusi wamekana madai hayo na kuyatuhumu mataifa hayo kwa kutengeneza tukio hilo ili kuhalalisha hatua za kijeshi. Kundi la Hezbollah la nchini Lebanon, mshirika wa serikali ya Syria, limelaani mashambulizi hayo na kusema mataifa hayo hayatatimiza malengo yake.

Kiongozi wa kidini mwenye ushawishi mkubwa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameyalaani mashambulizi hayo ya Syria na kuzitaja Marekani, Uingereza na Ufaransa wahalifu. Maafisa wa jumuiya ya kujihami ya NATO wamesema nchi hizo tatu zitawaarifu wanachama leo kuhusu mashambulizi hayo ya kijeshi yaliyofanya Syria.

Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa/Reuters

Mhariri: Sylvia Mwehozi