1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ana wasiwasi na utolewaji sawa wa chanjo ya COVID-19

23 Novemba 2020

Viongozi wa nchi za G20 wamesema watafanya kila linalowezekana kuhakikisha usambazaji sawa wa chanjo ya virusi vya corona, lakini Kansela Angela Merkel ameonyesha wasiwasi juu ya mchakato huo kwenda taratibu. 

https://p.dw.com/p/3lhDh
Deutschland | PK nach virtuellem G20 | Angela Merkel
Picha: Hannibal Hanschke/AP Photo/picture alliance

Katika mkutano wa kilele wa siku mbili ulioandaliwa na Saudi Arabia na kufanyika kwa njia ya vidio, mataifa tajiri zaidi ulimwenguni yaliahidi rasilimali ili kusaidia kushughulikia janga la virusi vya corona na kuunga mkono mataifa maskini ambayo uchumi wake umeathiriwa vibaya na mgogoro huo.

Kansela Merkelamesema ana wasiwasi kwamba hakuna makubaliano makubwa ya chanjo ambayo yamefikiwa na mataifa maskini hata wakati nchi tajiri zikinunua dozi kubwa kutoka makampuni ya dawa.

"Sasa tutazungumza na kundi la muungano wa chanjo ya dunia GAVI juu ya lini mazungumzo haya yataanza, kwasababu nina wasiwasi kwamba hakuna jambo lililofanyika. Wakati pesa ikiwepo yote basi tutaona na Ujerumani mara chache huwa haifanyi kitu lakini Ujerumani haiwezi kuunga mkono jumuiya ya kimataifa peke yake", alisema Merkel.

Kauli yake imekuja wakati mataifa tajiri yakiahidi kushughulikia mahitaji ya kifedha kuunga mkono uzalishaji na usambazaji sawa wa chanjo ya COVID-19, matibabau na vipimo. Katika mkutano na waandishi wa habari waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Mohammed al-Jadaan alisisitiza kuwa kulikuwa na maafikiano miongoni mwa kundi hilo la G20 akiongeza kuwa hakuna nchi itakayoachwa nyuma.

G20 Gipfel Saudi Arabien | Gruppenfoto digital
Mkutano wa G20 uliofanyika kwa njia ya vidioPicha: Pressestelle G20 Gipfel Saudi Arabien

"G20 iko na nia ya kuzisaidia nchi maskini, kuunga mkono uchumi huu kwasababu tunaamini kwamba kama tutaacha nchi yoyote nyuma, sote tunabaki nyuma. kwa hiyo tunahitaji kufanya kazi kwa pamoja na tumefanikiwa katika kushirikiana kuunga mkono jamii hizi na nchi", alieleza waziri wa mambo ya kigeni wa Saudia.

Wito unazidi kuongezeka kwa kundi la G20 kusaidia kuziba pengo la ufadhili wa dola bilioni 4.5 katika utaratibu unaoongozwa na shirika la afya duniani WHO, ambao unakusudia kuhakikisha upatikanaji wa vipimo, matibabu na chanjo kwa watu wote."Ufadhili zaidi unahitajika" alisema rais wa Halmshauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, akiongeza kwamba ameyataka mataifa ya G20 kuziba pengo hilo ifikapo mwishoni mwa mwaka. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliwataka wenzake "kwenda mbali zaidi na haraka" kwa kutoa dozi, kuunda ushirikiano wa kiviwanda na kushirikiana hakimiliki za uvumbuzi.

Hata hivyo kuna wasiwasi kwamba nchi kama Uingereza, Marekani , Ujerumani na Ufaransa tayari zimefanya mazungumzo ya moja kwa moja na makampuni ya madawa, ikimaanisha kwamba kiwango kikubwa cha chanjo tayari kimechukuliwa.

Rais Donald Trump alihudhuria kwa ufupi wakati wa ufunguzi wa mkutano huo na kusifu mafanikio ya "kihistoria" ya utawala wake na akasema kwamba anatazamia kufanya kazi na rais ajaye wa G20 ambaye atakuwa ni Italia wakati akikataa kukubali  kushindwa katika uchaguzi wa rais.