1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ala kiapo kuiongoza serikali ya Ujerumani

Oumilkheir Hamidou
14 Machi 2018

Kansela Angela Merkel anaanza mhula wake wa nne madarakani bila ya uungaji mkono kamili wa wabunge wa vyama vinavyounda serikali ya muungano.Takriban kila mbunge mmoja kati ya 11 hakumpa kura yake Angela Merkel. 

https://p.dw.com/p/2uK7H
Deutschland Vereidigung der Bundeskanzlerin
Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Baada ya kukabidhiwa na rais wa shirikisho Frank-Walter Steinmeier hati ya kuiongoza  serikali mpya ya muungano, Angela Merkel alirejea tena bungeni na kula kiapo mbele ya spika wa bunge la shirikisho Wolfgang Schäuble na wabunge waliohudhuria hafla hiyo kama kifungu nambari 56 cha sheria msingi ya Ujerumani kinavyosema. 

 "Nnaapa nitatumia nguvu zangu zote kwaajili ya ustawi wa wananchi wa Ujerumani, kuowaazidishia manufaa, kuwaepushia madhara, kulinda na kuihami sheria msingi na sheria za shirikisho, majukumu yangu kuyatekeleza kwa dhati na kuhakikisha haki sawa kwa wote. Na Mungu anisaidie," amenukuliwa Merkel wakati akila kiapo.

Mawaziri nao waapishwa

Baada ya kansela Merkel kuapishwa wakaapishwa  pia mawaziri wake . Wizara ya fedha na mambo ya nchi za nje zinashikiliwa na wanasiasa wa SPD,Olaf Scholz na Heiko Maas. Wizara ya mambo ya ndani inadhibitiwa na aliyekuwa waziri mkuu wa jimbo la Bavaria, Horst Seehofer wa chama cha CSU na wizara ya uchumi inaaoongozwa na mwanasiasa wa CDU,Peter Altmeier.

Deutschland Wahl der Bundeskanzlerin
Rais Frank-Walter Steinmeier akimkabidhi Merkel hati ya kuongoza serikaliPicha: picture-alliance/dpa/B. Von Jutrczenka

Mawaziri wengi wanaelezea utayarifu wao wa kuanza haraka majukumu yao. Kikao cha kwanza cha mawaziri kinafanyika leo jioni. Ratiba halisi haijulikani lakini kansela Merkel alisema alipoulizwa kuhusu kipa umbele cha serikali mpya tunanukuu "Kila kitu ni muhimu." Waziri wa kilimo Julia Klöckner anapanga kuzungumza na mabwanashamba wa Ujerumani kuhusu fidia zinazotolewa na Umojua wa ulaya. Waziri wa familia Franziska Giffey anasema anataka kwanza kulishughulikia suala la umaskini miongoni mwa watoto.

Kansela Merkel pia anapanga kwenda Paris wiki hii kwa mazungumzo pamoja na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuhusu mageuzi ya Umoja huo.

Licha ya kutoungwa mkono na wabunge wote 399 , vyama ndugu vya kihafiidhina vinayataja matokeo ya zoezi la kumchagua kansela bungeni kuwa ni ya kuridhisha na hasa kwa kutilia maanani ugumu wa kuunda serikali uliojitokeza. Mkuu wa kundi la wabunge wa chama cha SPD Andrea Nahles anaesema ameshangazwa na matokeo hayo anayoyataja kuwa ni haba.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP/Reuters/

Mhariri: Iddi Ssessanga