1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aanzisha mazungumzo ya kuunda serikali na SPD

Sekione Kitojo
7 Januari 2018

Zaidi ya miezi mitatu baada ya uchaguzi nchini Ujerumani, Kansela Angela Merkel bado anahangaika kuunda serikali mpya na Jumapili(07.01.2018)anazindua mazungumzo ya kukishawishi chama cha SPD kujiunga na serikali yake.

https://p.dw.com/p/2qS2l
Deutschland Spitzentreffen Union und SPD
Picha: Getty Images/A. Berry

Chama cha  SPD kwa  shingo  upande kilikubali kufanya mazungumzo ya awali ya uchunguzi na kinajivuta na  kuonesha "nyodo" na  kwamba  mazungumzo  hayo  hayatakuwa  rahisi. Kukivutia chama  hicho  kushirikiana  nacho ni kamari anayocheza Merkel katika  kuunda  serikali  imara  na  kurefusha  uongozi  wake wa  miaka  12 baada  ya  juhudi  zake  kuunda  ushirika  na  vyama viwili  vidogo kushindwa  mwaka  jana.

Berlin Statement SPD-Vorsitzender Schulz zu GroKo
Kiongozi wa chama cha SPD Mrtin SchulzPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Chama  cha  SPD , ambacho  kilishiriki  kutawala  katika  kile kinachoitwa  "muungano  mkuu" pamoja  na  vyama  vya  kihafidhina vinavyoongozwa  na  Merkel  kwa  miaka  minne  iliyopita, kimeapa kuingia  katika  upinzani  baada  ya  kupata  matokeo  yake  mabaya kabisa  tangu  mwaka  1933 lakini  kilitafakari  upya  msimamo  wake huo baada  ya  rais  kuingilia  kati.

Upinzani dhidi ya  muungano  huo katika  serikali  ni  mkubwa  katika SPD, kundi  linaloitwa "NoGroko" ikiwa  na  maana  "Hapana kwa muungano  mkuu", limeundwa  miongoni mwa  wanachama  kufanya kampeni  dhidi  ya  kufanya kazi  pamoja  na  Merkel  tena, likisema kwamba  hali  hiyo  itakigharimu  chama  cha  SPD  kupoteza  kura na  kukifanya  chama  cha  siasa  kali  za  mrengo  wa  kulia  cha Alternative for Germany   AfD kuwa  kiongozi  wa  upinzani.

Deutschland Spitzentreffen beim Bundespräsidenten
Angela Merkel akitoka kutoka mazungumzo ya matayarishoPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

"Hatupaswi  kufanya mambo  yaonekana  mazuri  kuliko  yalivyo, chama  cha  SPD  kina shaka kubwa  juu ya  kurejewa kwa muungano  huo  mkubwa," mwanachama  mwandamizi  wa  SPD Manuela Schwesig  amesema  katika  mahojiano  na  redio  ya Ujerumani  Deutschlandfunk radio.

Muungano  mkuu 

Norbert  Roemer , kiongozi wa  SPD katika  bunge  la  jimbo  la North Rhine - Westphalia , aliiambia  kampuni  ya  magazeti  ya RND  kwamba  hakuna  wabunge  kutoka  jimbo  lake  wanapendelea muungano  huo  mkuu - tofauti  na  miaka  minne  iliyopita, kutokana na  uzoefu  uliokuwapo  hapo  kabla  ikiwa  na  maana  hawamuamini tena  Merkel.

Berlin - Steinmeier lädt zu GroKo-Gesprächen ein | Martin Schulz
Martin Schulz akitoka katika mazungumzo ya matayarishoPicha: Imago/Future Image/B. Kriemann

Wazo  la  muungano  mkuu, kwa  kawaida  ni chaguo  la  mwisho kwa kuwa  linaufanya  upinzani  kuwa  na  wabunge  wachache, na  hilo haliungwi  mkono  na  wengi, ambapo uchunguzi  wa  maoni  kwa  ajili ya  kituo  cha matangazo  cha  ARD  umeonesha  zaidi  ya  nusu  ya Wajerumani , asilimia  52 wana shaka  wakati asilimia  45 wanapendelea.

Vyama  hivyo  bila  shaka  vitapambana  kuhusiana  na  suala  la uhamiaji, kodi, matibabu  na  Ulaya. Volker Bouffier , mwanachama mwandamizi  wa  chama  cha  Merkel  cha  Christian Democratic CDU , ameliambia  gazeti  la  Rheinische Post kuwa  chama  chake kinakusudia  kuunda  serikali  ya  muungano  mkuu.

Lakini  aliongeza: "Iwapo  hilo litafanikiwa bado haijulikani. Haiwezi kutokea  kwa  gharama  yoyote."

Kiongozi  wa  wabunge  wa  SPD  bungeni  Andrea Nahles alionesha ishara  ya  maridhiano  zaidi, akisema  hatachora  mistari  yoyote myekundu kabla  ya  mazungumzo, akiliambia  gazeti  la  Bild am Sontag, kwamba "Majadiliano yana  maana  hutapata mafanikio  ya asilimia  100  ya  madai  yako."

SPD Parteitag in Berlin - Andrea Nahles
Kiongozi wa wabunge wa SPD bungeni Andrea NahlesPicha: Getty Images/AFP/O. Andersen

Serikali mpya wakati wa Pasaka

Iwapo  majadiliano  yatakuwa  ya  mafanikio, serikali  mpya  huenda ikawepo ifikapo  wakati  wa  sikukuu  ya  Pasaka, amesema.

Horst Seehofer , kiongozi  wa  chama  cha  Christian Social Union CSU  chama  ndugu  na  chama  cha  kansela  Merkel  cha  CDU , amesema  ana  matumaini  vyama  vitakubaliana  kutawala  kwa pamoja, akisema : "Nafikiri tutaweza."

Washirika  hao  wamekubaliana  kutotoa  taarifa  wakati  wa mazungumzo  hayo  ya  matayarisho, ambayo  yanatarajiwa kumalizika siku  ya  Alhamis. Iwapo watapata  msimamo  wa  pamoja wa  kutosha na  chama  cha  SPD  kinapata  uungwaji  mkono kutoka  kwa  wanachama  wake  katika  kura , vyama  hivyo vitaendelea  na  mazungumzo  kamili  ya  kuunda  serikali.

Deutschland CSU Parteitag in Nürnberg
Kiongozi wa chama cha CSU Horst SeehoferPicha: Reuters/M. Dalder

Lakini  iwapo  majadiliano  yatashindwa, taifa  hilo  lenye  uchumi mkubwa  barani  Ulaya  huenda  likakabiliwa  na  uchaguzi  mpya, ama  kwa  mara  ya  kwanza  katika  enzi  za  baada  ya  vita, serikali yenye  wingi  mdogo  bungeni  chini  ya  Merkel  itaundwa.

Mazungumzo  yaliyoshindwa mwaka  jana  ya   kuunda  serikali yalihusisha  vyama  vya  kihafidhina  vinavyoongozwa  na  Merkel , pamoja  kile  kinachopendelea  wafanyabiashara  cha  Free democrats FDP  na  chama  cha  walinzi  wa  mazingira  The Greens.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre

Mhariri: Caro Robi