1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbunge ataka kifungo wapenzi wa jinsia moja kuondoshwa Ghana

16 Februari 2024

Mbunge mmoja nchini Ghana, Alexander Afenyo-Markin, amelitaka bunge la nchi hiyo kuondosha hukumu ya kifugo cha jela kwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja na badala yake wapewe adhabu zisizohusisha kufungwa.

https://p.dw.com/p/4cUl9
Wapenzi wa jinsia moja wakiunga mkono kutambuliwa Kenya.
Wapenzi wa jinsia moja wakiunga mkono kutambuliwa Kenya.Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Mbunge huyo aliyeshauri adhabu mbadala kujumuisha ushauri nasaha kwa wale watakaotiwa hatiani kwa makosa hayo, alisema muswaada dhidi ya watu hao wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, ambao kwa sasa uko bungeni, utachochea visa zaidi vya ulawiti magerezani.

Afenyo-Markin wa chama tawala cha Ghana alisema siku ya Alhamis (Februari 15) kwamba kufungwa jela kwa watu hao kunafanya hali kuwa mbaya zaidi na kuharibu lengo halisi la muswada huo.

Soma zaidi: Maaskofu Afrika wapinga kuwabariki wapenzi wa jinsia moja

Muswada huo ambao uko katika hatua yake ya mwisho kabla ya kuidhinishwa kuwa sheria, pia unawahimiza wale wanaotuhumiwa kwa kushiriki mapenzi ya jinsia moja kufanyiwa kile kinachofahamika kama "tiba ya kubadili jinsi" inayodaiwa kubadilisha utambulisho wa jinsia, ili nao wapunguziwe vifungo.

Tayari vitendo vya mapenzi ya jinsia moja katika taifa hilo la Afrika Magharibi ni kosa linaloloweza kupelekea adhabu ya hadi miaka mitatu jela kwa anayetiwa hatiani.