1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Sudan yagonga mwamba

8 Juni 2012

Mazungumzo baina ya Mawaziri wa Ulinzi kutoka Sudan na Sudan Kusini yamevunjika bila ya kufikia muafaka katika kikao maalum mjini Addis Ababa, Ethiopia.

https://p.dw.com/p/15Aao
Wanajeshi wa Sudan Kusini
Wanajeshi wa Sudan KusiniPicha: dapd

Mkutano wao uliitisha kujadili masuala ya ulinzi na usalama mipakani mwao kutokana na kuibuka kwa migogoro kadhaa iliosababisha mapigano baina ya mataifa hayo jirani.

Wakiwa katika kikao hicho cha kutatua mgogoro huo kuliibuka lawama za muda mrefu kwa kila upande kudai kuwa unasaidia waasi wa upande mwingine. Huku kukiwa hakuna makubalino juu ya eneo la mpakani lililopigwa marufuku kuweka silaha la kilomita 1800.

Mji wenye utajiri wa mafuta waHeglig.
Mji wenye utajiri wa mafuta waHeglig.Picha: AP

Hakuna kilichofikiwa ata juu ya ushuru wa usafirishaji wa mafuta katika mabomba ya mafuta na juu ya mapipa 350,000 ya Sudan Kusini yaliyochukuliwa na Sudan. Pia mjumbe wa Sudan katika kikao hicho ameilaumu Sudan Kusini kwa kudai kuwa eneo lenye utajiri wa mafuta la heglig kuwa ni lake

Sudan yailaumu Kusini

Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Ulinzi wa Sudan Abde Raheem Mohammed Hussein amesema ramani ya mipka inayotumika sasa ni ile ya makubalino yaliyofikiwa 2005 ambapo pande zote ziliafikiana lakushangaza Sudan Kusini ina madai mengine ya maeneo mapya matano.

Waziri huyo ameongeza kuwa mwaka 2009 ilitolewa hukumu na mahakama ya Usuluhishi ya Mjini The Hague juu ya jimbo la Abyei na maamuzi hayo yaliyotolewa yailonyesha kuwa Heglig ipo Kaskazini.

Wajumbe wa Sudan Kusini wapo kimya

Mpaka sasa Sudan Kusini hawajasema neno juu ya mazungumzo hayo kugonga mwamba lakini wakati wa ufunguzi wa mkutano huo

Heglig kabla ya mapigano
Heglig kabla ya mapiganoPicha: AP

Pagan Amun mjumbe wa serikali ya Sudan Kusini aliyekuweko Addis Ababa alisema." Mkutano wetu ulitupia jicho kuwepo utaratibu wa kuweka mikakati ya usimamizi wa mipaka baina ya nchi zetu mbili, pia kuunda kamati ya kupokea malalamiko ya pande zote mbili kama kukiwa na upande mmoja umekiuka makubalino ya mipaka yaliyofikiwa."

Mkutano huu, ulibarikiwa na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, AU, huku wajumbe kutoka pande zote na viongozi wakuu walikutana ili kuepusha kutokea kwa mapigano.

Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika wamezipa Sudan muda wa miezi miwili, hadi Agosti 2, ziwe zimeshapata suluhu juu ya mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuainisha mpaka wa kila moja, usafirishaji wa mafuta na masuala ya uraia.

Jopo la mazungumzo walikubali kutekeleza kikamilifu azimio namba 2046 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na mpango wa Umoja wa Afrika.

Sudan na Sudan Kusini zilipigana vita kwa muda mrefu na mwaka jana Sudan Kusini ikapata uhuru wake na kuwa taifa huru, lakini mwaka huu nchi hizo mbili ziliingia katika mapigano mara baada ya Sudan Kusini kuuteka Mji wenye utajiri wa mafuta wa Heglig, na baadae Sudan kuwafurusha askari walikuwepo katika mji huo na kusababisha vifo vya askari wengi katika mapigano hayo.

Mpaka sasa watu zaidi ya milioni 2 wamefariki katika mgogoro huo wa kiitikadi, kikabilia, kidini na kuwania mafuta

Mwandishi:Adeladius Makwega/RTRE

Mhariri: Mohammed Abdul-rahman