1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kati ya Upinzani na jeshi yafutiliwa mbali Sudan

Amina Abubakar Josephat Charo
30 Julai 2019

Viongozi wa maandamano Sudan wamefutilia mbali mazungumzo yaliyopangiwa kufanyika kati yao na majenerali wa kijeshi wanaoiongoza nchi, huku mamia ya wanafunzi wakishiriki maandamano kupinga mauaji ya wanafunzi wenzao

https://p.dw.com/p/3N1I2
Sudan Khartum Massenproteste der Opposition
Picha: Getty Images/AFP/E. Hamid

Wanafunzi hao waliyovalia sare zao za shule na kubeba bendera ya nchi yao Sudan, walisema kwa sauti "kumuua mwanafunzi ni sawa na kuliua taifa” wakati walipoandamana Mashariki mwa mji wa Burri kupinga mauaji ya wanafunzi wenzao watano waliouwawa kwa kupigwa risasi wakati wa maandamano dhidi ya uhaba wa mkate na mafuta nchini humo. 

Maandamano mengine pia yalifanyika katika maeneo tofauti katika mji Mkuu wa KhartoumWaandamanaji walililaumu jeshi linaloogopewa  kwa mauaji ya wanafunzi hao.

Sudan, Unruhen
Baadhi ya waandamanaji Sudan mjini Khartoum Picha: Getty Images/H. E.-Tabei

Mauaji hayo yalitokea siku moja kabla ya viongozi wa  maandamano kufanya mazungumzo na jeshi juu ya sehemu iliyobakia ya kurejesha utawala wa kiraia baada ya pande hizo mbili kukubaliana kugawana madaraka mapema mwezi huu.

Lakini Taha Osman mpatanishi anaetokea vuguvugu la maandamano amesema mazungumzo hayo kamwe hayatofanyika hii leo maana kundi lao bado lipo Al Obeid na litarejea hii leo usiku.

Mpatanishi mwengine aliliambia shirika la habari la AFP kwamba mazungumzo hayo yatarejea pindi patakapokuwa na utulivu, maana mazungumzo ndio njia pekee ya kupata suluhu ya mgogoro wa kisiasa unaolikumbwa taifa hilo kwa sasa.

Jeshi lalaani mauaji ya wanafunzi Sudan

Kwa upande wake mwenyekiti wa Baraza la kijeshi linaloiongoza Sudan Jenerali Abdel Fattah al Burhan ameyalaani mauaji ya wanafunzi hao watano.

"Kile kilichotokea Al-Obeid kinasikitisha, kuua raia ni uhalifu usiyokubalika unaohitaji uajibikishwaji wa haraka," alisema mwenyekiti huyo alipozungumza na waandishi habari.

Sudan Militärrat Abdel Fattah al Burhan
Mwenyekiti wa Baraza la kijeshi linaloiongoza Sudan Jenerali Abdel Fattah al BurhanPicha: picture-alliance/AA

Huku hayo yakiarifiwa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF limeitolea wito serikali ya Sudan kufanya uchunguzi wa mara moja juu ya mauaji ya watoto hao na kuwawajibisha wote waliyohusika. 

Madaktari wanaofungamanishwa na vuguvugu la maandamano wamesema  zaidi ya watu 250 wameuawa hadi  sasa katika maandamano yaliyogeuka na kuwa vurugu tangu mwezi Desemba wakati maandamano ya kwanza kabisa yalipoibuka dhidi ya rais aliyeondolewa Omar al Bashir.

Baraza la kijeshi limekuwa likishikilia madaraka nchini Sudan tangu jeshi hilo lilipomuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu nchini humo Omar al Bashir mnamo Aprili 11.

Vyanzo: afp/Reuters