1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya nyuklia ya Iran yaanza

14 Aprili 2012

Mazungumzo juu ya mpango tata wa nyuklia wa Iran yameanza leo (14.03.2012) baada ya kusimama kwa miezi 15 huku kukiwa na taarifa za kuwepo kwa matumaini hafifu ya kufikia muafaka baina ya pande mbili zinazojadiliana.

https://p.dw.com/p/14dsn
Rais Mahmoud Ahmedinejad wa Iran.
Rais Mahmoud Ahmedinejad wa Iran.Picha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa vyanzo vilivyo karibu na mazungumzo hayo baina ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani vimesema kwamba matumaini pekee ni kuwa mazungumzo ya leo yatazalisha mazungumzo mengine ndani ya wiki chache zijazo.

Uingereza, China, Ufaransa, Urusi, Marekani pamoja na Ujerumani, wote wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanakutana uso kwa uso na ujumbe wa Iran mjini Istanbul.

Kauli ya hivi karibuni ya Iran mahususi kwa mazungumzo hayo ilisema kuwa nchi hiyo imejiandaa kukaa katika meza ya majadiliano ya mpango wake wa nyuklia na mataifa hayo. "Kwetu sisi siku hii (Jumamosi) ni kama ya majaribio," alisema mjumbe mmoja kati ya wanaohudhuruia mazungumzo hayo mara baada ya kikao.

"Hatutarajii kupata taarifa nyingi zaidi lakini inawezekana tukakutana tena katika kipindi cha wiki 4 hadi 6 zijazo kama tutaweza na wakati huo ndipo tutakapozungumza kwa kina," alisema mwanadiplomasia mmoja kwa sharti la kutotajwa jina lake.

Shaka ya Jumuiya ya Kimataifa

Wasiwasi mkubwa wa jumuiya ya kimataifa ni kuongezeka kwa uwezo wa Iran wa kurutubisha madini ya yuraniumu ambayo yanaweza kutumika katika uzalishaji wa umeme na matumizi mengine ya amani, lakini kama itarutubishwa zaidi inaweza kutumika kutengeza silaha za kinyuklia.

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton (kushoto) na mpatanishi mkuu wa Iran katika mazungumzo ya nyuklia, Saeed Jalili.
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton (kushoto) na mpatanishi mkuu wa Iran katika mazungumzo ya nyuklia, Saeed Jalili.Picha: AP

Wasiwasi huo hasa upo katika eneo la siri la zamani la Fordo katika milima iliyopo kartibu na mji mtakatifu wa Qom, ambalo kwa sasa linarutubisha yuraniumu kwa kiasi cha asilimia 20. Lakini wataalamu wanasema kuwa lina uwezo wa kurutubisha madini hayo hadi kiwango kinachofaa kuzalisha silaha za nyuklia kwa kiasi cha asilimia 90.

Kukua kwa Fordo, pamoja na ripoti ya Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki Novemba mwaka jana juu ya juhudi za kuzuia utengenezaji wa silaha za nyuklia zimechangia kuweko kwa vikwazo vikali vya sasa vya Umoja wa Ulaya na Marekani dhihi ya Iran ambavyo vimechangia ukali wa bei ya mafuta ya nchi hiyo na kitisho cha Israel kuivamia kijeshi.

Iran imesema kuwa itapendekeza mipango mipya katika mkutano huo wa Istanbul. Israel na Marekani zimetishia kuchukua hatua za kijeshi kuizuia nchi hiyo kutengeneza silaha za nyuklia, hatua ambayo imechochea kupanda kwa bei za mafuta kwa asilimia 18 mwaka huu. Lakini Iran yenyewe inasema kuwa mpango wake huo wa nyuklia ni kwa ajili ya kuzalisha umeme na kwa matumizi ya kitabibu.

Mwandishi: Stumai George/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef