1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya China na Marekani "muhimu"

24 Agosti 2018

Mazungumzo ya kibiashara kati ya China na Marekani yameanza tena wiki hii huku China ikisema hii leo kwamba mikutano hiyo ilikuwa yenye umuhimu. Hata hivyo kumekuwa na muendelezo wa hatua za kuongezeana ushuru baina yao.

https://p.dw.com/p/33ga5
US-China-Handelsgespräche
Picha: Reuters/D. Lawder

Hata hivyo kumekuwa na muendelezo wa hatua za kuongezeana ushuru baina ya mataifa hayo, huku kukiwa hakuna mafanikio yoyote yaliyoanza kuonekana. 

Wizara ya biashara ya China imesema hii leo kwamba ilifanya mikutano iliyoieleza kuwa ni "yenye umuhimu" na maafisa wa Marekani baada ya mazungumzo yaliyoanza upya kati ya mataifa hayo kuhusiana na mzozo unaoendelea wa kibiashara.

Hata hivyo, huku kukiwa hakuna hatua zozote za kimaendeleo zilizoanza kuonekana, na kuanza kwa mazungumzo hayo hakukuzuia kuwekwa kwa ushuru mpya wa nyongeza wa dola bilioni 16, uliowekwa na Marekani na China kwa kila bidhaa zinazotoka na kuingia kwenye nchi hizo, kuanzia Alhamisi hii.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika siku ya Jumatano na Alhamisi yalilenga kuepusha kusambaa kwa mzozo wa kibiashara ulioibuka kati ya China na Marekani, na kushuhudiwa hatua za kuwekeana ushuru wa kulipizana kisasi wa dola bilioni 50 kwa bidhaa za mataifa hayo, lakini kukitarajiwa hatua zaidi. 

Shirika la habari la China, Xhinua limeripoti kwamba, maafisa wa pande zote wameahidi kuendeleza mawasiliano, huko mbeleni, kwa ajili ya awamu nyingine ya mazungumzo.

Cui Tiankai China Botschafter
Balozi wa China nchini Marekani, Cui Tiankai, amesema hakuna namna nyingine zaidi ya kuendeleza mashirikiano.Picha: picture-alliance/Zumapress

Balozi wa China nchini Marekani, Cui Tiankai hii leo amesema katika hafla iliyoandaliwa na gavana wa Kentucky Matt Bevin kwamba mashirikiano ndio chaguo pekee katika kuimarisha mahusiano ya kiuchumi kati ya China na Marekani, ambayo kwa wote yamekuwa ya kimaslahi miongoni mwa mataifa hayo.

Alinukuliwa akisema "Sisi ni mataifa mawili yenye nguvu zaidi kiuchumi duniani, lakini pia ni wanachama wa kudumu wa baraza la uslama la Umoja wa Mataifa. tuna jukumu kubwa si tu kwa mataifa yetu, lakini kwa dunia nzima. Na tuna mahitaji ya pamoja yanayozidi kuongezeka, na maslahi ya pamoja. Kwa hiyo haya yote yanahitimisha kwamba ushirikiano ndio namna pekee, namna bora pekee tunayotakiwa kuichukua."

Makubaliano hayo ya ngazi ya chini yalikuwa ya kwanza kufikiwa tangu mataifa hayo mawili yenye nguvu zaidi kiuchumi duniani yalipoanza kuwekeana ushuru wa kisasi wa mabilioni ya dola mnamo mwezi Juni. Ikulu ya Marekani ilisema mazungumzo hayo yalihitimishwa baada ya maafisa kubadilishana mawazo kuhusu namna watakavyofikia haki na usawa wa mahusiano ya kiuchumi. 

Mazungumzo hayo yalifanyika katika wizara ya fedha ya Marekani, ambapo maafisa hao wa Marekani walikutana na ujumbe wa china ulioongozwa na naibu waziri wa biashara na naibu mwakilishi katika makubaliano ya biashara za kimataifa Wang Shouwen. Ujumbe wa Marekani uliongozwa na David Malpass, chini ya waziri wa mahusiano ya kimataifa.

Masoko ya fedha ya Asia kwa kiasi kikubwa yameelezwa kushuka, baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo kati ya Marekani na China, wakati dola ya Marekani ikipanda, kabla ya hotuba ya mkuu wa benki kuu. Dola ya Australia ilianguka vibaya zaidi, katika wakati ambapo taifa hilo likiwa limegubikwa na sintofahamu ya kisiasa.

Mwandishi: Lilian Mtono/dw

Mhariri:Iddi Ssessanga