1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya biashara kati ya Marekani na China

Oumilkheir Hamidou
30 Januari 2019

Marekani na China wanaanza duru tete ya mazungumzo kuhusu biashara huku kukiwa na matumaini finyu ya kufanikiwa kutokana na masharti ya viongozi wa mjini Washington kulazimisha mageuzi katika mfumo wa kiuchumi wa China.

https://p.dw.com/p/3CQGP
USA China Symbolbild Wirtschaftskrieg
Picha: imago/C. Ohde

Pande hizo mbili zitakutana si mbali na ikulu ya Marekani kwa mazungumzo ya ngazi ya juu kabisa kuitishwa tangu rais Donald Trump na rais wa China Xi Jinping walipokubaliana Desemba iliyopita, kipindi cha siku 90 cha utulivu katika vita vyao vya biashara.

Kwa miezi kadhaa sasa mvutano wa kibiashara umekuwa ukiendekea huku kukiwa na maoni tofauti yanayotolewa na rais Trump kupitia mtandao wa Twitter, mara yakiwa ya kutia moyo  na mara nyengine ya vitisho. Wiki iliyopita tu Rais Trump alisema ameridhika na jinsi mazungumzo yalivyoendelea hadi sasa. Amesema ana hakika "China inapendelea sana kufikia maridhiano.

Kampuni la China Huawei
Kampuni la China HuaweiPicha: picture-alliance/NurPhoto/J. Arriens

Matumaini hafifu ya kufikiwa makubaliano

Matamshi kinyume na hayo lakini yalitolewa na waziri wake wa biashara Wilbur Ross ambae hatarajii makubaliano yoyote kufikiwa katika mvutano wa biashara pamoja na China. "Tuko mbali mno na kufikia maridhiano" amenukuliwa Ross akisema siku chache zilizopita, lengo likiwa kufifiisha matumaini yaliyoko. Muda si muda akasawazisha na kuzungumzia nafasi nzuri iliyoko ya kufikiwa maridhiano katika mazungumzo pamoja na ujumbe wa watu 30 kutoka Jamhuri ya Umma wa China.

Lakini uamuzi wa mahakama ya Marekani kulishitaki kampuni mashuhuri la teknolojia Huawei na kiongozi wake wa shughuli za fedha bibi Meng Wanzhou unahatarisha nafasi ya kufikiwa makubaliano yoyote yale.

Mjumbe wa Marekani katika mazungumzo ya biashara pamoja na China, Robert Lighthizer
Mjumbe wa Marekani katika mazungumzo ya biashara pamoja na China, Robert LighthizerPicha: Reuters/J. Lee

Kipindi cha utulivu kinamalizika Machi inayokuja

Wachina wanaongozwa na makamo waziri mkuu Liu He ambae tayari ameshawasili Washington tangu jumatatu iliyopita. Wanakutana kwa majadiliano kuanzia leo pamoja na mjumbe wa Marekani anaeshughulikia masuala ya biashara Robert Lighthizer na waziri wa fedha Steven Mnuchin. Kesho wamepangiwa pia kukutana na rais wa Marekani Donald Trump.

Wakati unayoyoma kwa sababu makubaliano yaliyofikiwa kati ya rais Trump na mwenzake wa China Xi Jinping ya kutuliza vita vyao vya kibiashara muda wake unamalizika mwezi Machi unaokuja. Pindi makubaliano yakishindwa kufikiwa hadi wakati huo, Rais Trump anapanga kutangaza ushuru ziada dhidi ya bidhaa zote zinazoingizwa Marekani kutoka China  zenye thamani ya hadi dola bilioni 500 .

Mwandishi:Kohlmann,Thomas/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Gakuba, Daniel