1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo baina ya Marekani na Urusi kuhusu usalama wa anga

Saleh Mwanamilongo
27 Julai 2020

Maafisa wa serikali za Marekani na Urusi wamekutana mjini Vienna,Austria, ili kuendesha mazungumzo kuhusu usalama wa anga baada ya shutuma dhidi ya Moscow.

https://p.dw.com/p/3g09u
Marekani na nchi za Ulaya zaishutumu Urusi kufanya jaribio la silaha za teknolojia ya anga za juu.
Marekani na nchi za Ulaya zaishutumu Urusi kufanya jaribio la silaha za teknolojia ya anga za juu.Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Silva

Maafisa wa serikali za Marekani na Urusi wamekutana mjini Vienna,Austria, ili kuendesha mazungumzo kuhusu usalama wa anga baada ya Washington na London kuishutumu Moscow kufanya jaribio  wiki iliyopita la silaha za teknolojia ya anga za juu.

Mazungumzo hayo ya siku moja yaliyoandaliwa kwa miezi kadhaa, yatafuatiwa na kikao cha siku tatu kuhusu udhibiti wa silaha za nyuklia baina ya nchi mbili hizo.

Christopher Ford, naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani anayehusika na maswala ya kiusalama alisema Ijumaa iliyopita kwamba ''Urusi na China zimegeuza anga kuwa eneo la mapambano''.

Ford aliendelea kusema kwamba Marekani inapendekeza kanuni za mwenendo wa kuwajibika kuhusu matumizi ya anga. Kanuni hizo zitalingana na zile za kivita zilizoko hivi sasa ambazo zinahusu maadili ya uwiano na ya ubinadamu, aliwaambia wandishi wa habari.

Urusi yakanusha shutuma

Urusi ilifanya jaribio la satelaiti ndogo.
Urusi ilifanya jaribio la satelaiti ndogo.Picha: Reuters/ARMS Courtesy CSIS Asia Maritime Transparency Initiative/DigitalGlobe

Kwenye mkataba wa kimataifa, Urusi na China ziliunga mkono juhudi za kila mmoja katika kuzuia matumizi ya silaha kwenye anga.Ford alisema kwamba Marekani ilipinga pendekezo hilo kwa sababu linapiga marufuku mfumo wa silaha maalumu ambazo ni vigumu kuzieleza, pahali pa kuelezea kuhusu vitendo vinavyohitajika angani.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya anga ya Marekani ni kwamba Urusi ilifanya jaribio, katikati ya mwezi Julai, la silaha  za teknolojia ya juu,lililofanana na jaribio lingine la taifa hilo mwaka 2017.

Urusi ilikanusha shutuma hizo. Wizara ya mambo ya nje ya Urusi ilielezea Ijumaa kwamba jaribio lilihusu satelaiti ndogo ya uchunguzi wa kifaa cha anga cha Urusi kinachotumia masafa mafupi.

Kwa upande wake Dmitri Peskov,msemaji wa ikulu ya Kremlin,alisema kwamba Urusi itaendelea kuhakikisha kwamba lengo la kutokuweko na silaha na kutotuma aina yoyote ya silaha angani limetekelezwa.