1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maysasa ataka mazungumzo na vyama vya upinzani kuhusu Brexit

17 Januari 2019

Serikali ya Uingereza imesema waziri mkuu Theresa May yuko tayari kufanya mazungumzo mapya juu ya mkataba wa kuiwezesha Uingereza kuondoka kwenye Umoja wa Ulaya itakapofika tarehe 29 mwezi Machi.

https://p.dw.com/p/3BjUv
Kombobild May - Corbyn

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema atafanya mazungumzo ya busara na viongozi wa vyama  vya upinzani pamoja na wabunge kwa moyo wa kuleta mafanikio na kutafuta njia ya kusonga mbele ili Uingereza iweze kuondoka Umoja wa Ulaya. Serikali yake imethibitisha kwamba ikifika Jumatatu itaweza  kuuwasilisha mpango mbadala wa Brexit na kwamba wabunge watapewa fursa ya siku nzima ya kuujadili  na kuufanyia marekebisho endapo itabidi tarehe 29 mwezi huu.

Hata hivyo pamekuwapo na ishara finyu juu ya kupiga hatua kwenye mazungumzo na viongozi hao wa upinzani baada ya kiongozi  wa chama kikuu cha upinzani  cha Labour,Jeremy Corbyn kuyaita mazumgumzo hayo kuwa ni usanii wa maonyesho. Akizungumza kwenye mji wa Hastings, Corbyn amemtaka waziri mkuu May aonyeshe dhamira ya kweli juu ya mapendekezo  yanayohusu hali ya baadae. Kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani Jeremy Corbyn amesema hatakutana na waziri mkuu ikiwa May hataondoa uwezekano wa Uingereza kutoka kwenye Umoja wa Ulaya bila ya mkataba.

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Reuters

Na mbunge wa chama cha kijani Caroline Lucas aliekutana na waziri mkuu May amesema kiongozi huyo anaishi katika dunia ya kubuni kwa kufikiria kwamba mkataba wa Brexit unaweza kubadilishwa hadi hapo Jumatatu. May bado anaushikilia msimamo wake wa kujiondoa kwenye soko la pamoja la umoja wa forodha.

Wakati huo huo nchi za Umoja wa Ulaya zinaimarisha matayarisho ya kujiweka sawa endapo Uingereza itaondoka Umoja wa Ulaya bila ya mkataba, baada ya bunge la Uingereza kuukataa mkataba ambao bibi  May aliuwasilisha kwenye bunge hilo.

Waziri wa Mambo ya nje Heiko Maas amesema Ujerumani itafanya kila inaloweza katika siku zijazo kuhakikisha kwamba makubaliano yanafikiwa wakati ambapo Uingereza inajiondoa kutoka Umoja wa Ulaya. Maas pia amesisitiza kwamba kutokana na kuendelea kwa mivutano katika bunge la nchini Uingereza kuhusu mchakato wa Brexit chini ya miezi mitatu kabla ya nchi hiyo kuondoka rasmi hapo Machi 29, Ujerumani itaongeza kasi katika maandalizi endapo kutatokea mchakato wa Brexit ambao utakuwa nje ya mpango uliotarajiwa.

Mwandishi:Zainab Aziz/AP/RTRE/AFPE

Mhariri:Iddi Ssessanga