1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

May kukutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya kuhusu Brexit

Mohammed Abdulrahman
17 Oktoba 2018

Juhudi hizo zinalenga kuepusha uwezekano wa Uingereza kujitoa mwezi Machi, bila ya kufikiwa makubaliano na Umoja wa Ulaya

https://p.dw.com/p/36iMN
Belgien | Beginn EU-Gipfel mit Beratungen zum Brexit
Picha: Reuters/Y. Herman

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May anatarajiwa kukutana  na viongozi wenzake 27 wa Umoja wa Ulaya  mjini Brussels baadaye leo, kukiwa na juhudi mpya za kuondoa hali ya mkwamo katika mazungumzo ya kujitoa kwenye Umoja huo, mchakato unaojulikana kama Brexit. 

Juhudi hizo zinalenga kuepusha uwezekano wa Uingereza kujitoa mwezi Machi, bila ya kufikiwa makubaliano na Umoja wa Ulaya.

Siku kumi za mazungumzo  marefu kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza zilifikia kikomo Jumapili ilipodhihirika kwambapande hizo mbili hazitoweza kuyakamilisha kwa ufanisi kabla ya  mkutano wa kilelewa wiki hii. Suala kuu la mabishano ni mpaka wa Ireland. Mjini  Berlin, akilihutubia bunge la Ujerumani Bundestag leo kabla ya kuelekea Brussels leo,  kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema:

" Nina tumai kwamba pamoja na kujitoa  Umoja wa Ulaya , lakini Uingereza  itaendelea kubakia kuwa mshirika wa karibu na wa kuaminika."

Suala kuu la mabishano ni mpaka wa Ireland.
Suala kuu la mabishano ni mpaka wa Ireland.Picha: Reuters/Y. Herman

Mnamo siku ya Jumanne kiongozi wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo ya Brexit Michel Barnier aliyaambia mataifa wanachama  kwamba  amependekeza kurefushwa  muda wa kipindi cha mpito cha Uingereza cha miezi 21 kwa mwaka mmoja zaidi na kwamba Uingereza iendelee kuwa chini ya sheria za Umoja wa Ulaya. Alisema kipindi  hicho kitaweza kutoa muda zaidi wa kujadili uhusiano wa siku zijazo baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya, na ambayo yatasaidia kupiga hatua kuhusu suala la  mpaka wa Ireland , la kutorudi tena katika utaratibu wa ukaguzi katika mpaka wa Jamhuri ya Ireland na Ireland Kaskazini pale Uingereza itakapojitoa.

Waziri mkuu May amepanga kuonana na  rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya  Donald  Tusk, Rais wa  halmashauri kuu ya Ulaya Jean-Claude Juncker na Waziri mkuu wa Jamhuri ya Ireland Leo Varadkar mjini Brussels baadae leo kabla ya kuanza mkutano wao wa kilele. Jioni hii (17.10.2018) atawahutubia viongozi wenzake 27, kabla ya wao kula chakula cha usiku, lakini bila ya bibi May .

 

Mhariri: Josephat Charo