1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

May akutana na Tusk kujadili kuhusu Brexit

1 Machi 2018

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May Alhamisi hii amemualika rais wa Umoja wa Ulaya, Donald Tusk kwa mazungumzo juu ya mpango wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja huo.

https://p.dw.com/p/2tXPk
Großbritannien London - Theresa May und Donald Tusk
Picha: Getty Images/AFP/D. Leal-Olivas

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May hii leo amemualika rais wa Umoja wa Ulaya, Donald Tusk kwa mazungumzo juu ya mpango wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja huo, Brexit, ikiwa ni siku moja kabla ya kutoa hotuba yake itakayohusu mustakabali wa mahusiano ya kibiashara kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya, katika wakati ambapo kuna mvutano mkali kuhusu suala la Ireland Kaskazini. 

Mkutano wao ambao umefanyika katika ofisi ya waziri mkuu May,katika mtaa wa Downing , unakuja wakati ambapo Umoja wa Ulaya nao ukiandaa msimamo wao kuhusu mustakabali wa kimahusiano na Uingereza, baada ya taifa hilo kujiondoa. 

May kwa upande wake, pia yuko tayari kuweka wazi mipango yake katika hotuba iliyosubiriwa kwa muda mrefu hapo kesho, ingawa hata hivyo imekuwa ikikabiliwa na kiza kinachosababishwa na mvutano na Umoja wa Ulaya kuhusu hadhi ya mpaka na Ireland Kaskazini baada ya Brexit.

Wiki hii, Umoja wa Ulaya ulichapisha rasimu ya sheria inayoelezea makubaliano ya talaka yaliyofikiwa na Uingereza mnamo mwezi Disemba, ambayo ni pamoja na mikakati ya kuepusha vikwazo vyovyote vinavyotokana na ukaguzi wa ushuru wa forodha katika mpaka kati ya Ireland Kaskazini na Ireland.

Donald Tusk aitaka Uingereza kuja na wazo mbadala.

May akiwa na ghadhabu alilizungumzia pendekezo kwamba Ireland Kaskazini ambayo ni sehemu ya Uingereza itaendelea  kubaki katika mpango wa pamoja wa ushuru wa forodha na Umoja wa Ulaya, iwapo hakutakuwa na suluhu nzuri zaidi, huku akionya kutokukubaliana na suala lolote litakalotishia uadilifu wa katiba ya nchi yake.  

Großbritannien Kampagne gegen den Brexit
Uingereza imeendelea na mazungumzo na Umoja wa Ulaya ya kujiondoa kutoka kwenye Umoja huo.Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Dunham

Kwenye hotuba yake mjini Brussels mapema hii leo, kabla ya kuelekea London Tusk alisema iwapo waziri mkuu May hakupenda wazo hilo, anatakiwa kuja na wazo mbadala. 

Lakini pia Tusk aliukosoa mtazamo wa Uingereza kwenye makubaliano hayo kuhusu mustakabali wa mbele wa kimahusiano, akisema mipaka iliyojiwekea yenyewe ilisababisha matarajio yake ya kuwa na biashara isiyokuwa na msuguano kutowezekana.  

Awali, Rais huyo wa Umoja wa Ulaya alisema ana uhakika kabisa kwamba mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya wataikubali rasimu ya mkataba wa makubaliano ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja huo, ambao hata hivyo umeibua ghadhabu nchini Uingereza, kutokana na kipengele kinachoihusu Ireland Kaskazini. 

Ireland na Umoja wa Ulaya kwa pamoja wametoa mwito kwa makubaliano yoyote ya Brexit kuepusha ugumu wa mpakani, ili kulinda makubaliano ya mwaka 1998 yaliyojulikana kama Good Friday Agreement, yaliyofikiwa Ireland Kaskazini, ambayo yalihitimisha miongo mitatu ya mapigano mabaya zaidi ya kimadhehebu.

Mkataba wa makubaliano ya Brexit wenye kurasa 120, unaweka katika nakala ya kisheria maelezo kuhusu vipengele vya makubaliano yaliyofikiwa mwezi Disemba na waziri mkuu wa Uingereza, Theresa May na rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Junker. 

Hapo jana, May alilikataa pendekezo la Umoja wa Ulaya, linaloiruhusu Ireland Kaskazini kusalia kwenye mpango wa pamoja wa ushuru wa forodha na Umoja wa Ulaya, hivyo kuipa nafasi ya kuendelea kufanya biashara kwa uhuru na Jamhuri ya Ireland, lakini likiweka mpaka kati ya Ireland Kaskazini na maeneo yaliyosalia ya Uingereza.

Mwandishi: Lilian Mtono/afpe/dpae.
Mhariri:Yusuf Saumu