1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Nje wa ECOWAS wakutana kuijadili Senegal

8 Februari 2024

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi za Afrika Magharibi wanafanya mazungumzo ya dharura leo wakikabiliwa na mgogoro wa kisiasa nchini Senegal na watawala wa kijeshi katika nchi tatu zilizokumbwa na mapinduzi.

https://p.dw.com/p/4c9xw
Baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS).
Baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS).Picha: Kola Sulaimon/AFP

Kikao hicho maalum cha Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) kinafuatia uamuzi wa ghafla wa Rais Macky Sall kuahirisha uchaguzi wa Senegal, wiki moja tu baada ya Burkina Faso, Mali na Niger kutangaza kuwa wanajiondoa katika jumuiya hiyo.

Baraza la Upatanishi na Usalama la ECOWAS limesema mawaziri watakutana katika mji mkuu wa Nigeria Abuja leo kujadili hali ya sasa ya usalama na masuala ya kiasasa katika kanda hiyo.

Haikufahamika jana kama waziri yeyote wa Senegal atahudhuria. ECOWAS imeihimiza Senegal - moja ya mataifa wanachama wake wenye utulivu - kurejea katika ratiba yake ya uchaguzi, lakini wakosoaji tayari wametilia shaka mwelekeo wa kundi hilo juu ya nchi wanachama wanaozidi kukaidi.