1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Mazingiza wa nchi 50 kukutana nchini DRCongo

1 Oktoba 2022

Mawaziri wa mazingira wa takriban nchi 50 watakusanyika siku ya Jumatatu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa mazungumzo ya kuandaa Mkutano wa hali ya hewa wa COP27 utakaofanyika nchini Misri.

https://p.dw.com/p/4HcfY
Felix Tshisekedi | Präsident Demokratische Republik Konogo
Picha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

Mazungumzo hayo yasiyo rasmi katika mji mkuu wa nchi hiyo ya Afrika ya kati, Kinshasa yanakuja kabla ya mkutano wa kilele wa hali ya hewa wa COP27 utakaofanyika Sharm El Sheikh nchini Misri, kuanzia Novemba 6 hadi 18. Mawaziri na wajumbe wengine wanatarajiwa kujadili mambo ambayo yanaweza kusababisha vikwazo katika mkutano mkuu ujao.

Mpatanishi wa hali ya hewa wa nchi ya Kongo Tosi Mpanu Mpanu ameliambia Shirika la habari la AFP kuwa hakuna tangazo rasmi linalotarajiwa kutolewa katika mkutano huo.

Mwanadiplomasia wa Magharibi, ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema kwa vile mikutano yote miwili ya hali ya hewa itafanyika barani Afrika, swala litakalotiliwa maanani ni uungwaji mkono kutoka kwa nchi zilizoendelea kiviwanda kuelekea Mataifa yanayoendelea.

Mada hiyo pia ilikuwepo pia wakati wa mazungumzo ya hali ya hewa ya COP26 ya mwaka 2021 huko Glasgow, ambayo yalimalizika kwa ahadi ya kuheshimu kiwango cha joto duniani kisichozidi nyuzi joto 1.5 kipimo cha Celcius.

Soma zaidi: Mataifa tajiri yaahidi fedha za kuisaidia Afrika kukabiliana na tabianchi

Shinikizo la nchi zinazoendelea

Eco Africa | Sendung 29.04.2022 | Spanien
Kisiwa kimoja nchini Senegal kikikabiliana na mafuriko Picha: DW

Nchi maskini zaidi zilikuwa zimeshinikiza kuwepo kwa utaratibu wa kuzingatia uharibifu unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Lakini mataifa tajiri ambayo ndio wachafuzi wakuu wa mazingira, walikataa wito huo na washiriki walikubali badala yake kuanzishwe "mazungumzo" juu ya ufadhili wa uharibifu huo.

Misri ambayo ndio mwenyeji wa mkutano wa 27 wa Hali ya hewa (COP27), imesema kuwa tayari kushiriki katika mkutano huo wa mjini Kinshasa utakaomalizika siku ya Jumatano.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inatarajiwa kujinadi kama nchi inayoweza kutoa suluhu za mabadiliko ya hali ya hewa wakati wa mazungumzo hayo. Ikiwa na ukubwa unaokaribia kuwa sawa na eneo la Ulaya Magharibi, Kongo ina jumla ya ekari milioni 395 za msitu wa mvua ambao hutumika kama hifadhi ya hewa chafu ya kaboni.

Soma zaidi: Mnada wa vitalu vya mafuta nchini DRCongo ni hatari kwa mazingira

Kongo pia ina akiba kubwa ya madini kama vile cobalt na lithium, ambazo zinachukuliwa kuwa muhimu kwa matumizi ya mpito kuelekea nishati mbadala na pia katika uzalishaji wa betri.

Kinshasa inaomba ufadhili zaidi ili kulinda misitu yake ya mvua, ambayo kwa sasa inatishiwa na kilimo kutokana na maeneo hayo kufyekwa na kuchomwa pamoja na ukataji miti kwa ajili ya uzalishaji wa mkaa.

Mkutano wa wanasayansi

Demokratische Republik Kongo | Gerodeter Wald nahe Kisangani
Msitu uliofyekwa karibu na Kisangani nchini DRC.Picha: SAMIR TOUNSI/AFP/Getty Images

Kabla ya mkutano huo wa kabla ya kongamano la COP27, serikali ya Kongo iliandaa mkutano na wanasayansi katika Hifadhi ya Mazingira ya Yangambi katika msitu wa kaskazini mashariki, uliyomalizika kwa wito wa wanasayansi kuitaka jumuiya ya kimataifa "kuunga mkono mipango yote" ya kulinda msitu wa mvua. Dieu Merci Asumani ni Mkurugenzi wa shirika la Inera:

" Jamii ya wenyeji inahitaji kuwa na shughuli mbadala, shughuli zinazopunguza shinikizo kwenye msitu. Lakini mifumo ya jumuiya ya kimataifa bado ni ya kinadharia sana, kuna taratibu ndefu sana za kupata "fedha za ufadhili wa kaboni". Hii leo tunafikiri kwamba nchi zinazochafua zaidi mazingira ndizo zinazoendelea kutajirika zaidi kuliko zile ambazo zinafanya jitihada za kukabiliana na athari za hali ya hewa kwa kusalia na kiwango cha nyuzi joto 1.5 kipimo cha Celsius."

Mada inayohusiana: 

DRC yatoa leseni za utafiti wa mafuta na gesi kwa vitalu 30

Hata hivyo, wito huo unajiri baada ya serikali mwezi Julai kupiga mnada vitalu 30 vya mafuta na gesi, ikipuuza maonyo kutoka kwa wanaharakati watetezi wa mazingira walisema kuwa kuchimba visima ni hatari kwa misitu ya mvua na ardhi inayotumika kama hifadhi ya hewa chafu ya kaboni na hivyo kupelekea kusambaa kwa kiasi kikubwa cha hewa chafuzi kwa mazingira.

Watafiti walikadiria katika utafiti wa mazingira mwaka 2016 kuwa takriban tani bilioni 30 za kaboni zimehifadhiwa katika Bonde la Kongo, idadi hiyo ikiwa ni sawa na miaka mitatu ya uzalishaji wa hewa chafu kote duniani.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo ni moja mwa nchi maskini zaidi duniani, inasema kuwa uchimbaji wa mafuta na gesi unaweza kusaidia uchumi wake na kuwanufaisha watu wa Kongo.