1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wawaziri wa mazingira wakikubaliana mpango wa uwekezaji

Reuben Kyama17 Septemba 2021

Mkutano wa mawaziri kutoka Afrika wanaoshughulikia mazingira (AMCEN) umekamilika mjini Nairobi, wakikubaliana kuwa na mpango kamili wa kuongeza uwekezaji.

https://p.dw.com/p/40T1Y
Uganda tropischer Bergregenwald
Picha: C. Kaiser/blickwinkel/picture alliance

Mawaziri kutoka zaidi ya nchi hamsini barani Afrika walijumuika pamoja kwa njia ya mtandao katika kikao cha kumi na nane cha kongamano hilo. Katika kilele cha mkutano huo hapo jana Alhamisi, chini ya udhamini wa Shirika la kimataifa la uhifadhi wa mazingira, UNEP, wajumbe walifikia maamuzi muhimu ya kuelekea mkutano wa Glasgow.

Selemani Saidi Jafo ni Waziri wa Mazingira kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tungependa kuthibitisha kujitolea kwetu kama serikali ya Muungano wa Tanzania katika jitihada za kutetea ajenda inayodhamiria kuhifadhi mazingira ulimwenguni. Tayari tumeanza kuandaa kampeini kabambe tunapojiandaa kushiriki kwenye mkutano wa 26 wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (COP26). Kwa kweli tungetaka kuudhihirishia ulimwengu kwamba sisi kama Waafrika tuko tayari kuyatunza mazingira.

Athari ya Covid-19 kwa uchumi wa Afrika

Kwa hakika, inatupasa kuyajali mazingira yetu ili kuweza kuishi kwa amani.
Kwa hakika, inatupasa kuyajali mazingira yetu ili kuweza kuishi kwa amani.Picha: DW

Kikao hicho cha mawaziri wa mazingira barani Afrika kimefanyika ikiwa imesalia takribani mwezi mmoja tu kabla ya kufanyika kwa mkutano wa 26 wa kimataifa wa kujadili mabadiliko ya tabiachi, utakaoandaliwa mwezi Novemba mwaka huu Mjini Glasgow, nchini Scotland.

Akihutubia  kikao hicho kwa njia ya mtandao, Waziri wa Misitu na Maliasili wa Malawi, Nancy Tembo, amesema mataifa ya bara la Afrika yanakabiliwa na kipindi kigumu kiuchumi na kijamii kutokana na makali ya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19. 

Mlipuko wa ugonjwa huu umetukumbusha kwamba japo mazingira ni muhimu kwa maisha yetu kuna uwezekano wakati mwingine yanaweza kutuathiri endapo hatutozingatia umuhimu wa kuyahifadhi na kuyatunza ipasavyo. Kwa hakika, inatupasa kuyajali mazingira yetu ili kuweza kuishi kwa amani.

Wakati wa kikao hicho, wasemaji wakiwepo pia wakuu kutoka Shirika la UNEP wamepitisha uamuzi mwafaka wa kubuni mpango kabambe wa kushughulikia mazingira barani Afrika.