1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa ASEAN wakutana Laos

Josephat Charo
24 Julai 2024

Nchi za jumuiya ya Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN, zimekutana hivi leo mjini Viantiene nchini Laos huku zikipania kuendeleza juhudi za kuutanzua mgogoro nchini Myanmar na mzozo wa bahari ya China Kusini.

https://p.dw.com/p/4iekT
Mawaziri wa kigeni wa China, Japan, Korea Kusini
Mawaziri wa mambo ya kigeni wa China, Japan, Korea Kusini walipokutana katika mkutano wa ASEAN Jakarta Indonesia mwaka 2023Picha: Yonhap/picture alliance

Nchi za jumuiya ya Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN, zimekutana hivi leo mjini Viantiene nchini Laos huku zikipania kuendeleza juhudi za kuutanzua mgogoro nchini Myanmarna kutuliza wasiwasi kuhusu suala la bahari ya China Kusini.

Mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi wanachama wa jumuiya hiyo watajadili mkwamo katika juhudi za kuufikisha mwisho mgogoro ambao umegeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Myanmar ambao Umoja wa Mataifa unasema imewalazimu watu milioni 2.6 kuyakimbia makazi yao.

Wanachama wakubwa wa jumuiya ya ASEAN zikiwemo Thailand, Indonesia, Singapore na Malaysia zimekatishwa tamaa na hatua ya utawala wa kijeshi kutokuwa tayari kutimiza ahadi zake kufanya mdahalo, hali ambayo imeiweka katika mtihani uaminifu na uwezo wa jumuiya hiyo kutekeleza mpango wa amani uliokubaliwa miezi kadhaa baada ya mapinduzi ya mwaka 2021.

Mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje utafuatiwa na mikutano miwili ya kilele mjini Laos siku ya Jumamosi inayolenga kushughulikia masuala ya kimataifa, utakaohudhuriwa na maafisa kutoka Marekani, Umoja wa Ulaya, Japan, China, urusi na kwingineko.