1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa ASEAN wakutana huko Laos

25 Julai 2024

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa ASEAN pamoja na wanadiplomasia waandamizi kutoka Marekani na China wanakutana leo hii katika jiji la Vientiane ambalo ni mji mkuu wa Laos.

https://p.dw.com/p/4iimV
Indonesien, Jakarta | 43. ASEAN Gipfel
Picha: Mast Irham/Pool/REUTERS

Mawaziri hao wanaanza mazungumzo ya siku tatu yanayotarajiwa kujikita katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Myanmar, mvutano katika eneo la Bahari ya China Kusini na masuala mengineyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Laos, Saleumxay Kommasith, alipoufungua mkutano huo, amewashukuru wanachama wa ASEAN na washirika wote kwa juhudi zilizoleta mafanikio makubwa huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza kazi ya kuhamasisha amani na utulivu.

Mazungumzo mapana yatakayowajumuisha pia wanadiplomasia wa eneo hilo ambao ni pamoja na Japan, Korea Kusini, India na Australia yanatarajiwa kuangazia zaidi masuala ya kiuchumi, usalama, mazingira na nishati.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken na Wang Yi wa China wanatarajiwa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana, pembezoni mwa mkutano huo unaofanyika wakati mataifa hayo mawili yakisaka kuongeza ushawishi kwenye ukanda huo.